Na Mwandishi Wetu,Kasulu
Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kupitia Idara ya Elimu Msingi imefanya kikao cha wadau wa elimu wa Kata ya Mvugwe na Makere kwa ajili ya kuweka mikakati ya ufaulu wa mitihani ya darasa la nne na darasa la saba kwa mwaka wa masomo 2025.
Kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni katika Shule ya Msingi Mvugwe kilihusisha wenyeviti wa kamati za shule,viongozi wa dini,viongozi wa serikali za vijiji,walimu,polisi kata,wazee maarufu na watu wa taaluma kutoka makao makuu ya halmashauri.
Akizungumza katika kikao hicho Mratibu wa Timu ya Ufuatiliaji, Respice Swetu amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kupata tathimini kwa ngazi ya kata ni mikakati ipi iwekwe ili kuongeza kiwango cha ufaulu.
“Hapa tunaangalia ni kitu gani kinatakiwa kufanywa kwakuwa mwaka uliopita tulikuwa wa kwanza kimkoa katika mitihani ya darasa la nne na wa pili kimkoa katika mtihani wa darasa la saba tukaona walimu ndio hasa waliotekeleza kazi hiyo wakishirikiana na wadau hivyo tupo hapa kushirikishana yanayotakiwa kufanyika ili mafanikio hayo tuliyopata yaimarike zaidi,” amesema.
Kwa upande wake Afisa Elimu Taaluma wa Halmashauri hiyo, Joseph Maiga amesema kuwa utekelezaji wa mikakati iliyowekwa ili iweze kuwa na mashiko ni lazima walimu wabaini kiwango cha uelewa baina ya wanafunzi ili waweze kwenda nao wote sambamba.
Mmoja wa washiriki wa kikao hicho,Mkebyela Elias amesema kuwa mikakati iwekwe ili suala la chakula liwe kwa madarasa yote na si tu yale ya mitihani kitu kitakachosaidia watoto kupenda shule na ufaulu kuongezeka.
Akifunga mkutano huo Diwani wa Kata ya Mvugwe, Mhe. Nuhu Abel amewataka wazazi kuacha dhana potofu ya kuwa chakula wananchochangia shuleni kinaenda kuwanufaisha walimu kitu kinachosababisha mara nyingi zoezi hilo kuzorota.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.