Na Mwandishi Wetu
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma,Vanica Ndelekwa siku ya jana amezindua zoezi la ugawaji miche ya Kahawa kwa wakulima katika Kata ya Buhoro wilayani humo.
Katika uzinduzi huo Ndelekwa amewataka wakulima kutoka katika kilimo cha chakula ambacho ndio wanachokifanya hivi sasa na kuhamia kwenye kile cha kibiashara kwa kulima zao la Kahawa.
-
“Sisi kilimo chetu kikubwa hapa Kasulu ni mahindi,mihogo na maharage ambayo si mazao ya biashara yale ni mazao ya chakula, tunauza tu kwasababu walaji wa vitu hivyo wamekuwa wengi ukiangalia halmshauri yetu kwa kiasi kikubwa hatuna zao la biashara tumebaki kung’ang’ana na mazao hayo matatu,” amesema.
Aidha, Vanica amewahakikishia wakulima hao kuwa zao la Kahawa soko lake ni la uhakika ambapo kilo inaanza shilingi 4000 hadi 6000 ndio maana imeanzishwa Amcos katika kata ya Buhoro kwa lengo la wao kuuza zao hilo hapo.
Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mickdadi Mbaruku ametoa angalizo kuwa soko la Kahawa linaanzia shambani hivyo mtu akichelewa kuivuna na kugeuka rangi hadi kuwa nyeusi thamani yake huwa inashuka.
Naye Mratibu wa zao hilo wilayani humo,Masumbuko Kelemwa amesema kuwa miche hiyo 174,000 itatolewa bure kwa kila mkulima atakayeihitaji sanjari na kutoa mafunzo ya kuipanda na kuikuza ili zao hilo liweze kuleta tija kwa walengwa.
Katika hatua nyingine Diwani wa Kata ya Buhoro,Mathiasi Sunzu amebainisha kuwa kutokana na zao hilo kuwa na uhakika wa soko anaiona kata hiyo kupiga hatua kubwa kwenye suala la maendeleo miaka michache ijayo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.