Na Mwandishi Wetu
Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani kiasi cha shilingi Bil 2.56 sawa na 104% tofauti na makisio ya awali yaliyokuwa shilingi Bil 2.4 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ulioanza Julai 1, 2023.
Mapato hayo yametokana na ushuru wa mazao, ukodishaji wa mashamba, ushuru wa huduma, uchangiaji wa huduma za afya na vyanzo vingine vya mapato.
Hayo yamebainishwa leo Juni 2, 2024 wilayani humo na Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo, Sarah Kibona alipozungumza na mwandishi wetu na kubainisha kuwa mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na ushirikiano mkubwa uliokuwepo kati ya halmashauri na wadau wake muhimu pamoja na viongozi wa Wilaya ya Kasulu.
Aidha, Kibona amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Dkt. Semistatus H. Mashimba kwa kuongeza mapato kwa 24% katika kipindi cha miezi miwili toka alipofika kutoka 80% hadi kufikia 104%.
“Mkurugenzi toka alipofika kwa kipindi kifupi alitilia mkazo suala la ufuatiliaji na kuimarisha doria ili kuzuia mianya ya upotevu wa mapato, amenunua mashine za kukusanyia mapato POS 40 na idadi yake kufikia 75 zilizosaidia walipa ushuru kuongezeka, kutolewa elimu na uhamasishaji kwa wakulima kujihusisha na kilimo cha chakula na biashara na utumiaji wa Mfumo Mpya wa Ukusanyaji Mapato Serikalini (TAUSI) kuhakikisha unatumika ipasavyo,” amesema.
Katika hatua nyingine Mweka Hazina amesema kuwa ana imani asilimia hiyo itaongezeka kabla ya mwaka wa fedha 2023/2024 kuisha kutokana na mikakati madhubuti iliyowekwa na kuwapongeza watumishi wote wa halmashauri hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya hadi mafanikio hayo kupatikana.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.