Halmashauri ya wilaya ya Kasulu inatarajia kupata mradi wa kujenga ustahimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi kwa wakulima wadogo wadogo kwa njia ya kilimo mseto katika wilaya za Uvinza na Kasulu yenye gharama za dola za kimarekani 1.5 sawa na shilingi za kitanzania bilioni 3.5
Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa katika tarafa nne zilizopo katika halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ambazo ni Heru chini, Buyonga, Makere na Buhoro kwa muda wa miaka 5 (2023-2028) miaka miwili ya upandaji miti na miaka mitatu ya usimamizi na mchakato wa biashara ya hewa ya ukaa
Watekelezaji wa mradi huu ni shirika lisilo la kiserikali la Marafiki wa Ziwa Tanganyika (FOLT) kushirikiana wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu likiwa na Lengo la kufikia wakulima wadogo wadogo wapatao 1250.
Akisoma taarifa yake ya utekelezaji wa Mradi huo Mkurugenzi Mtendaji wa FOLT Said Kasanula amebainisha kuwa jumla ya miti 2,635,000 itapandwa kwenye mashamba na kingo za mito kwa matumizi mbalimbali.
Mradi huu utachangia katika utekelezaji wa sera ya serikali ya upandaji miti pia kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya dunia hususani lengo la Hakuna umasikini, hakuna njaa pamoja na lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha mradi huu unatarajiwa kuwezesha kufanyika kwa bihashara ya hewa ya ukaa kupitia soko la hewa ya ukaa la hiari na hivyo kuongeza kipato kwa wakulima wadogo wadogo.
Kasanula aliongeza kuwa tafiti zinaonesha kuwa kilimo mseto cha kupanda miti kwenye mipaka ya mashamba tu na kile cha kuchanganya miti na mazao ya muda mrefu kinapunguza hewa ya ukaa ambayo huuzwa kwa dola za kimarekama 10-40 kwa tani moja.
Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kupitia mradi huo inatarajia kuboresha maisha ya wakulima wadogo wadogo na kuwajengea ustahimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi kupitia kilimo mseto ifikapo 2028
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.