Na Mwandishi Wetu
Ili kukabiliana na ugonjwa wa Malaria Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imetakiwa kuwasimamia vizuri watendaji wa kata na vijiji kwenye zoezi la uandikishaji wa kaya zinazotakiwa kupatiwa vyandarua kwakuwa kutakuwa hakuna vile vya ziada kwa zile ambazo taarifa zao hazitachukuliwa.
Mwakilishi wa Wizara ya Afya-Mpango wa Kudhibiti Malaria (NMCP), Peter Gitanya amebainisha hayo jana kwenye Mkutano wa Uraghibishaji kwa viongozi wa halmshauri hiyo la zoezi la ugawaji wa vyandarua kwa ngazi ya kaya bila malipo.
“Uandikishaji huu utatumia njia ya simu hivyo hakikisheni viongozi wa vijiji hawateuwi mwandikishaji kutoka kijiji kingine na hakutakuwa na chandarua chochote cha ziada kwa kaya ambayo haijajiandikisha kwahiyo ukitokea upungufu ni mtendaji wa kijiji kakaa chini na waandikishaji wake kaamua kutudanganya,” amesema.
Pia, amesema kuwa halmashauri itakuwa na jukumu la kuhakikisha usalama wa vyandarua wakati wa usafirishaji wake pamoja na kusimamia matumizi ya rasilimali fedha kama ilivyokusudiwa.
Naye Mwakilishi wa Mratibu wa Malaria OR- TAMISEMI,January Bonventure amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2025-2026 serikali imesisitiza upangaji wa bajeti katika halmashauri hiyo uelekeze nguvu nyingi katika kukabiliana na ugonjwa huo ili kusaidia unyunyiziaji wa dawa kwenye mazalia ya Mbu.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,Komesha Kaminyoge amebainisha kuwa watahakikisha wanahamasisha wananchi kujiandikisha katika kaya zao ili wote waweze kupata vyandarua kwa kutumia vyombo vya habari,matangazo kwenye masoko ya jioni,viongozi wa dini na watu maarufu.
Katika hatua nyingine Mratibu wa Malaria Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Dkt. Berlino Mlange amesema kuwa ugawaji wa vyandarua hivyo ni agizo la utekezaji wa afua za malaria kwa ngazi ya taifa ndio maana halmashauri kwa makadirio ya awali inategemea kugawa vyandarua vipatavyo 307,709.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.