Na Mwandishi Wetu
Ujumbe wa wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmshauri hiyo,Dkt.Semistatus H. Mashimba jana Mei 17, 2024 umefanya ziara ya kimafunzo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi kujifunza biashara ya Kaboni.
Akiongea katika tukio hilo Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Bruno Mwaisaka amesema biashara ya Kaboni inafanyika kwa namna mbili zinazojumuisha utengenezaji wa krediti au wahusika kuwa kama wateja.
“Sisi hivi sasa inatakiwa tuuze krediti ili tuweze kuwa na nguvu nazo tofauti na ukiwa kama mteja soko lake linakuwa si la uhakika kwa mfumo uliopo hivi sasa ni vizuri kutengeneza krediti ili uwe na uhakika wa kupeleka sokoni kwamba hiki nachokiuza kipo kwenye ubora,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Dkt. Semistatus H. Mashimba amesema kupitia ziara hiyo amepata weledi mkubwa wa ufanyaji wa biashara hiyo kwa kujua ni taasisi gani zinahusika, hatua zinazopaswa kufuatwa,muda unaochukua hadi kuanza biashara pamoja na changamoto zilizopo.
“Biashara ya Kaboni ni nzuri inatusaidia kutunza mazingira yetu changamoto zinakuja kutoka kwetu sisi wenyewe kwa baadhi ya maeneo kukataa kufanya mchakato wa namna bora ya kutunza misitu yetu inayotupa faida ya kufanya biashara ya Kaboni pamoja na mazingira yetu kuwa salama,” amesema.
Naye Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Sarah Kibona amesema kuwa mchakato wa kufanya biashara ya Kaboni ni mrefu na unahitaji fedha hivyo kwa bajeti zinazofuta wataweka kipaumbele katika kuwekeza katika biashara hiyo.
Katika hatua nyingine Kaimu Afisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Elkana Maige amebainisha kuwa hatua ya kwanza watakayofanya ni kukutana na kamati za utunzaji wa mazingira za vijiji ili kuanzisha mchakato wa usimamizi wa misitu ya vijiji yenye umuhimu kwenye utekelezaji wa biashara ya hiyo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.