HALMASHAURI Ya Wilaya Ya Kasulu imeonyesha kuwezekana kabisa kubadilisha changamoto kuwa fursa kwa kufanya kazi kubwa kupitia ukusanyaji wa pesa ndogo zitokanazo na mapato ya ndani endapo viongozi wa serikali watakuwa na uchungu katika usimamizi wa kutosha wa mapato hayo na dhamira ya dhati.
Aliyasema Hayo Mkuu Wa Mkoa Wa Kigoma Mhe. CGF (Rtd) Thobias Emir Andengenye alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika ufunguzi wa nyumba tano za kuishi watumishi wa Afya katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mnamo tarehe 26/01/2023.
Aidha alimpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia serikali anayoiongoza kwa kuweka sheria ya kutenga 40% ya mapato ya ndani kwaajili ya kufanyia shughuli zinazoonekana na kuimarisha huduma ambazo zinawagusa wananchi wote kama hospitali, shule na maji.
"Nichukue nafasi hii kuushukuru sana uongozi wa Halmashauri Ya Wilaya Ya Kasulu kwa mradi huu ambao kwanza ni maelekezo ya Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan lakini pili kwa kutumia pesa kidogo waliyonayo wametuonesha kumbe ukiwepo na usimamizi wa kutosha,kukiwepo na dhamira ya dhati, kukiwepo na uchungu kwa upande wa viongozi wa serikali inawezekana kabisa pesa kidogo zinazokusanywa kufanya kazi kubwa na kubadilisha changamoto kuwa fursa", alisema Mhe. andengenye
Mhe. Andengenye aliwasihi wananchi wa Halmashauri Ya Wilaya Ya Kasulu kuendelee kutoa ada, ushuru na tozo mbalimbali bila kukwepa kwani matunda yake yanaonekana kupitia ukamilishaji wa miradi na kuleta maendeleo yanayonufaisha jamii husika kwa ujumla
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Mhe. Kanali Issac Anthony Mwakisu aliwaomba wananchi wa Wilaya ya Kasulu kuendelea kuvumiliana na kufanya kazi kwa umoja kwa kuwa kazi moja walionayo ni kuhakikisha Kasulu inakwenda mbele na hakuna kiongozi alie na nia ya kuonea mtu bali kazi inafanyika kwa kufata maelekezo ya Serikali na kwaajili ya maslahi mapana ya nchi ya Tanzania.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa nyumba tano za Watumishi wa hospitali Mganga Mkuu Wa Hospitali Ya Halmashauri Ya Wilaya Ya Kasulu Dkt.Robert Nelson Rwebangira alisema Halmashauri hiyo inaendelea kupanua wigo wa huduma za afya kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya afya kwa lengo la kufikia maendeleo endelevu hasa Afya na hali bora kwa wananchi wote ifikapo 2030
Mradi wa nyumba tano umegharimu jumla ya shilingi 291,551,400 hadi kukamilika sawa na shilingi 58,310,280 kwa kila nyumba kwa awamu ya kwanza katika wamu ya pili ya ujenzi wa nyumba nne zenye uwezo wa kuhifadhi familia tatu, unatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi 535,373,852 sawa na shilingi 133,843,463 kwa kila nyumba ambapo inatarajiwa mradi utakapo kamilika kuhifadhi familia 17 za watumishi wa afya
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.