Na Mwandishi Wetu
Wananchi wilayani Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuunganisha nguvu kuwapinga wapiga ramli chonganishi maarufu kama Kamchape kwakuwa wanadhalilisha watu kupitia vitendo wanavyofanya.
Hayo yamebainishwa jana na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Michael Ngayalina alipofuturisha makundi mbalimbali ya watu katika wilaya hiyo.
Amesema wananchi wanapaswa kuhamka na kupambana na kundi hilo la kitapeli linaloibia watu kupitia mazingaombwe wanayofanya na kuwatuhumu watu kuwa ni wachawi na kujenga chuki katika jamii.
“Viongozi wa dini mliopo hapa sauti yenu itangulie mbele kwakuwa huwa mnaongoza jamii kwenye kutafsiri maandiko jukwaa lenu naliona lina nguvu hivyo tunaomba mtusaidie katika hili,” amesema.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kasulu, Mbelwa Chidebwe amesema wamejipanga kupita maeneo mbalimbali ya wilaya kukemea vitendo hivyo vya kihuni na kitapeli.
“Niwaombe wote tushikamane katika hili katika mwezi huu Mtukufu tumuombe Mungu kupitia dua zetu hatuepushe na hili kwakuwa ni shirki na katika imani yetu sisi Waislamu shirki ni dhambi ,” amesema.
Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa Wilaya Hiyo,Masoud Kukoba amefarijika kuona Futari hiyo imejumuisha watu kutoka nyanja tofauti kukaa pamoja kwa upendo na kuzitaka halmashauri zingine kuiga mfano huo.
Naye Mwenyekiti wa Makanisa ya Kipentekoste (CPCT) Wilaya ya Kasulu, Mchungaji Wilbert Muhoza amebainisha kuwa Mungu aliyetuumba kwa mfano wake huwa anafurahi kuona watu wa imani tofauti wanapokaa kwa pamoja na kusikilizana.
Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Emmanuel Ladislaus amesema kuwa dhamira ya Mkuu wa Wilaya kuandaa Futari hiyo ni kutaka kuchota sawabu zinazotokana na kufuturisha watu waliofunga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu,Vumilia Simbeye amesema tukio hilo limefanikiwa kutokana na serikali kuendelea kudumisha amani na utulivu miongoni mwa watu.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Mhe. Eliya Kagoma amebainisha kuwa Upendo na umoja unaoitambulisha nchi yetu katika anga la kimataifa umeoneshwa kwa vitendo kwa waudhuriaji wa tukio hilo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.