Na Mwandishi Wetu
Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) imeridhia jimbo la Kasulu Vijijini kugawanywa ili lipate kuwa na majimbo mawili ambayo ni Jimbo la Makere na Buyonga.
Kikao hicho kimefanyika leo Ijumaa Machi 14,2025 katika Ukumbi wa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Kanali Michael Ngayalina ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kasulu.
Akizungumza katika kikao hicho Kanali Ngayalina amesema kuwa jambo hilo ni la kisheria baada ya tangazo la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuhusiana na kubadilisha majina au kugawanya kwa majimbo.
”Kulingana na maelezo yaliyotolewa mchakato katika ngazi ya chini kabla ya mchakato wa ngazi ya wilaya umeshafanyika,kwahiyo leo kikao hiki kitapitia yale yaliyofanyika katika ngazi zilizotutangulia na sisi tukibariki mchakato huu ulioanzishwa tutapeleka mapendekezo yetu katika Baraza la Ushauri la Mkoa (RCC),” amesema.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Ndelekwa Vanica amesema kuwa ofisi yake kazi yake ni kutoa ushauri elekezi wa kitaalam ni njia gani za kupita ili mchakato huo upate kufanikiwa.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kasulu, Mbelwa Chidebwe amebainisha kuwa wameona kupitia madiwani na washauri mbalimbali kuligawa jimbo husika kutokana na ukubwa wa eneo na wingi wa watu.
Kwa upande wake Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vijijini, Simon Nzibuje amesema kuwa ugawaji wa jimbo utasaidia kurahisisha kuhudumia wananchi kwenye shughuli za uwakilishi kutokana na hivi sasa mambo kuwa magumu kutokana na ukubwa wa eneo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.