Na Mwandishi Wetu
Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma hapo jana imefanya ziara kukagua miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu na kuridhishwa namna jinsi inavyotekelezwa.
Akizungumza wakati wa ziara Makamu Mwenyekiti wa halmshauri hiyo, Laurent Poteza amesema kupitia ukaguzi waliofanya wamejiridhisha kuwa 99% ya miradi waliyopita imeweza kukidhi vigezo vilivyowekwa.
“Miradi ambayo tumeikagua leo (jana) zaidi ya 99% imekidhi vigezo kwakuwa ipo katika hali nzuri na sehemu za marekebisho tumetoa maelekezo kwa shule hivyo tunaamini kile tulichokielekeza kitafanyiwa kazi,” amesema.
Naye Diwani wa Kata ya Kurugongo, Edson Hanyuma amebainisha kuwa utekelezaji wa miradi hiyo imewagusa wananchi kwakuwa siku za nyuma ilipokuwa inafika mwanzo wa mwaka wananchi walikuwa wanatakiwa kutoa fedha kwa ajili ujenzi wa madarasa.
“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan ameleta fedha nyingi kwenye ngazi ya halmashauri nchini kote hasa katika sekta ya elimu kitu kilichosaidia wananchi kuepeukana na michango isiyo ya lazima,” ameongeza.
Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Iyogo Isuja amesema kuwa utekelezaji wa miradi ya ujenzi mashuleni ukumbana na changamoto ya vifaa kuchelewa kufika maeneo ya miradi hivyo watakabiliana nazo ipate kukamilika kwa wakati.
Kwa upande wake Muhandisi wa halmashauri hiyo, Valence Philemon amebainisha kuwa Idara ya Ujenzi imejipanga kuhakikisha miradi inayoendelea kutekelezwa inakamilika kwa wakati.
Pia, Diwani wa Kata ya Rungwe Mpya, Jonas Abilikaja ameshauri menejimenti ya halmshauri hiyo kuhakikisha ujenzi wa mabweni katika shule ya mchepuo wa kiingereza ya ‘Hope Pre and Primary’ kuanza haraka ili kuwavutia wateja walioko maeneo ya mbali.
Katika hatua nyingine Afisa Elimu Msingi (Takwimu), Sadick Lugagi amesema kuwa uanzishwaji wa shule ya ‘Hope Pre and Primary’ umelenga kukuza taaluma katika upande mwingine wa mtaala wa masomo unaotumia lugha ya kiingereza.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.