Na Mwandishi Wetu
Kufuatia maelekezo ya serikali kuzitaka mamlaka za halmashauri nchini kutenga asilimia kumi ya fedha zitokanazo na mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imeendelea kuwa kinara wa kutekeleza agizo hilo.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi pikipiki 15 zenye thamani ya shilingi milioni 40 kwa kikundi cha vijana cha "Twaweza" kutoka katika kata ya Makere, mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Eliyah Kagoma amewataka vijana waliopata mkopo huo kutumia nguvu na akili katika kazi yao.
Amewaambia kuwa pikipiki hizo hawajapewa bure hivyo zinatakiwa zitumike kama mtaji utakaowawezesha kupata pesa ili kurejesha gharama zilizotumika kununua pikipiki hizo na kujijengea imani kwa serikali.
Aidha amewataka vijana hao kuepuka kuzitumia pikipiki hizo katika matumizi maovu yakiwemo ya kuchepusha mapato ya halmashauri na kusafirisha wahalifu na badala yake waisaidie halmashauri kwa kutoa taarifa ya uchepushaji wa mapato kwa kuzingatia kuwa kutokana na kupewa mkopo huo, na wao sasa ni sehemu ya halmashauri.
"Mjue kuwa pesa za mkopo wa kununulia pikipiki hizo zimetokana na makusanyo ya ndani hivyo mkiona watumishi wa halmashauri wanakuja kukusanya ushuru, tozo na mapato mbalimbali toeni ushirikiano, huko ndiko zilipotoka pesa zilizonunua pikipiki hizo" amewaambia.
Akitoa maelezo kuhusu mkopo huo, Afisa Maendeleo ya jamii wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Victoria Makyao amesema kuwa, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2022 na 2023, halmashauri ya Wilaya ya Kasulu imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 208,000,000.
Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo, shilingi 95,000,000 zimetokana na makusanyo ya mapato ya ndani huku shilingi 113,000,000 zikiwa zimetokana na marejesho ya mikopo hiyo.
Makyao ameongeza pia kuwa kupitia pesa hizo, jumla ya vikundi 24 vimenufaika na kuvitaja vikundi hivyo pamoja na mikopo waliopata kuwa ni shilingi 87,000 zilitolewa kwa vikundi 13 vya wanawake, shilingi 95,000,000 zilitolewa kwa vikundi 8 vya vijana huku shilingi 26,000,000 zikienda kwa vikundi 3 vya watu wenye ulemavu.
Kuhusu hali ya marejesho, taarifa ya Makyao imeeleza kuwa, hadi kufikia Machi 30 mwaka huu, jumla ya shilingi 326,252,492 zimerejeshwa.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.