Na Mwandishi Wetu
Wakurugenzi wa serikali za mitaa, idara na taasisi za serikali na zisizo za kiserikali zinazohusika na kutoa elimu ya jinsia na uwekezaji kwa wanawake wametakiwa kuimarisha uratibu wa shughuli za elimu na hamasa ili kuleta mabadiliko ya kifikra katika ngazi ya jamii.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye ametoa agizo hilo leo kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kimkoa yalifanyika Kata ya Makere iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.
Amesema kwa kufanya hivyo itakuwa ndio njia pekee ya kuleta maendeleo ya haraka kwa taifa lakini ikiwemo kuimarisha ustawi wa jamii.
“Naagiza hamasa hii ifanyike katika ngazi zote za mamlaka za serikali za mitaa na zisimamiwe vizuri na idara zinazohusika hasa zile za maendeleo ya jamii,” amebainisha.
Aidha, amebainisha kuwa Mkoa wa Kigoma katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umeweza kupokea kiasi cha shilingi trilioni 11.450 kukabiliana na mambo mbalimbali yaliyofanya kuonekana kati ya mikoa yenye changamoto nyingi katika suala la maendeleo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu amesisitiza suala la ulinzi na usalama kwakuwa linasaidia wananchi kufanya shughuli zao za kimaendeleo bila bughudha yoyote.
“Mimi ni Mwenyekiti wa Usalama katika wilaya niwaombe wananchi wote wa Kasulu na mkoa kwa ujumla tuwekeze katika ulinzi na usalama kitu kitakachosaidia maendeleo tunayoyataka yaweze kufikiwa kwa urahisi,” amebainisha.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Eliya Kagoma akitoa neno katika maadhimisho hayo amesema kuwa upendo wa mama ni kitu kizuri kwakuwa hata ukitelekezwa na baba uhakika wa kuoga, kuvaa, kula pamoja na kusoma unakuwepo.
“Mimi nimefundishwa kusoma na mama yangu mzazi kwahiyo nilienda shule ya msingi tayari najua jambo hilo, nilikuwa nakaa naye akipika chakula jikoni namwambia mama sasa wanasomaje ananiambia ngoja nikufundishe,” amesema.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.