Jengo la madarasa mawili na Ofisi ya Mwalimu Mkuu katika shule ya Msingi Nyakasanda lililofunguliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kasulu, Mhandisi Godfrey Kasekenya leo tarehe 21.11.2018 katani Nyachenda.
Mkurugenzi wa Hmalmashauri ya Kasulu, Mha. Kasekenya (mwenye suti Nyeusi) akielekea kufungua mradi wa ujenzi wa madarasa na ofisi ya Mwalimu Mkuu katika shule ya Msingi Nyakasanda. Kushoto kwake ni Mratibu Elimu wa Kata ya Nyachenda Ngd. Jonas Donge.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Mha. Godfrey Kasekenya (wa kwanza kulia) akiwa katika Picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Halmashauri pamoja na Kata ya Nyachenda mara baada ya kukata Utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa majengo mawili ya madarasa pamoja na Ofisi katika Shule ya msingi Nyakasanda.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza wakati wa ufunguzi wa madarasa na Ofisi katika shule ya msingi nyakasanda, wakisikiliza hotuba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu mara baada ya ufunguzi wa jengo la Madarasa na Ofisi katani Nyachenda.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Kasulu, Mha. Kasekenya (aliye kaa katikati), akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa kijiji, kata na halmashauri, mara baada ya kukagua Ofisi ya Mwalimu Mkuu aliyoifungua pamoja na madarasa mawili katika shule ya msingi Nyakasanda iliyopo kwenye Kata ya Nyachenda wilayani hapa.
Na. Andrew Mlama-Kasulu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Mhandisi Godfrey Kasekenya, amefungua Mradi wa ujenzi wa madarasa mawili pamoja na ofisi ya Mwalimu mkuu katika shule ya Msingi Nyakasanda iliyopo kata ya Nyachenda wilayani hapa.
Mradi huo uliogharimu zaidi ya Shilingi Mil 15/ umezinduliwa leo tarehe 21.11.2018 katani hapo, ambapo fedha zilizotumika kutokana na thamani ya nguvu pamoja na michango ya wananchi ni jumla ya shilingi 10,018,600. na kiasi cha Shilingi 5,750,000 kimetoka katika Fedha za Mfuko wa Jimbo.
Akiongea na watumishi pamoja na wananchi waliojitokeza katika ufunguzi huo, Mhandisi Kasekenya amesema kuna masuala ya utekelezaji yanawezekana kutelekezwa na wananchi pale watakapoweza kusikilizana na kukubaliana kufanya kazi za maendeleo kwa pamoja wakitumia nguvu na fedha kidogo pamoja na kuishirikisha Serikali.
Amesema kuwa kuendana na hali halisi ya mahitaji ya Shule hiyo, bado kuna upungufu wa vyumba vya madarasa 15, nyumba za walimu 8, matundu ya vyoo 32, madawati 121. Wilaya itatoa msaada wa vifaa vya kiwandani pale ambapo nguvu za wananchi zitatumika na itaonekana kuna uhitaji wa Halmashauri kusaidia katika ukamilishaji wa miundo mbinu hiyo ya Elimu.
amesisitiza wakazi hao na jamii kwa ujumla kuongeza kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na utengenezaji wa madawati. “Kutokana na mfumo wa Elimu bure, kuna tarajio la uwepo wa wanafunzi wengi watakaohitimu Elimu ya Msingi na kujiunga na Kidato cha kwanza. Hali hii itapelekea hitajio kubwa la miundombinu hiyo ifikapo mwaka 2021” amesisitiza Kasekenya.
Ametoa Rai kwa wazazi kusitisha kuwatuma watoto wa kike kwenye masoko ya jioni au usiku na kuwapunguzia kazi za nyumbani ambazo hupelekea kuwashusha kitaaluma. “Utaratibu huo ndio chanzo cha Ajira ndogondogo za mitaani, aidha hupelekea watoto wengi kujikuta wakijiingiza katika tabia zisizofaa na hata kupelekea kupata mimba za utotoni” amesisitiza Mkurugenzi.
Amewaasa wakazi hao kuhakikisha wanaitunza Miundombinu hiyo ya kielimu. Aidha amesisitiza wazazi kufuatilia maendeleo ya kitaaluma na kuwahimiza watoto wao kuhudhuria shuleni kwa ufasaha huku wakishirikiana na walimu ili kutokomeza utoro wa rejareja na ule wa kudumu ambao ni chanzo cha kudidimia kwa Taaluma yao.
Diwani wa Kata ya Nyachenda Mh. William Luturi amemshukuru Mkurugenzi kwa ahadi yake kwa niaba ya Serikali kuhusu kusaidia umaliziaji wa Miradi inayotekelezwa na wananchi. Aidha amempongeza kwa uhimizaji, ushauri na usimamizi mzuri wakati wa ujenzi wa Miundombinu hiyo ya elimu “Mbegu uliyoipanda matunda yake yataonekana baada ya muda mfupi ujao kwani kwa Jicho la haraka hatuwezi kuiona faida yake kwa sasa ila baada ya kitambo kifupi tu. Mungu akujalie uendelee kuwepo ili na wewe ujionee Matunda ya kazi yako” amesema Luturi.
“Ujenzi huu tumeufanya kwa kuchangishana kwa hiyari ambapo kila kaya ilichangia shilingi 4000, pamoja na kutumia akiba ya matofali ya kijiji yaliyokuwepo kwa muda mrefu. Fedha zilizobaki tumezielekeza katika ujenzi wa Ofisi ya ulinzi ambao unaendelea kufanyika. Hii ni katika kuhakikisha tunaweka mazingira ya kijiji na kata katika hali ya usalama pia”amesisitiza Luturi.
Luturi ameushukuru uongozi wa kijiji pamoja na wananchi kwa kufanya kazi bila ugomvi wala kusukumana. Aidha amewasisitiza kuendelea kutekeleza miradi mingine ya Maendeleo kwa nguvu na umoja ili kutimiza malengo waliyojiwekea katika kuhakikisha wanatekeleza Miradi mbalimbali ya Maendeleo katani hapo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.