Na Mwandishi Wetu
Wakazi wa kijiji cha Chekenya kata ya Kurugongo wamepongezwa kwa ujenzi wa Zahati kubwa na ya kisasa ya kijiji chao ikiwa ni hatua muhimu ya kusogeza huduma za afya karibu na maeneo wanayoishi.
Pongezi hizo zimetolewa jana na wajumbe wa Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma walipofanya ziara katika kata hiyo iliyokuwa na lengo la kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza katika ziara hiyo Afisa Usafi na Udhibiti wa Taka wa halmashauri hiyo, Ndelekwa Vanica aliyemwakilisha Mkurugenzi, Joseph Kashushura ameitaka kamati ya ujenzi wa zahanati hiyo kuhakikisha inakuwa na taarifa zote muhimu za ujenzi tokea ulipoanza na kufikia kwa sasa.
Pia,ameitaka kamati hiyo ya ujenzi kuhakikisha mkandarasi wa mradi anafanya mawasiliano na wahandisi wa halmashauri kwa kila hatua inapokamilia ili wakague ubora wa jengo.
“Pamoja na hili la kukaguliwa na wahandisi wa halmashauri mkandarasi anatakiwa kuwa eneo la mradi kila wakati ili kubaini makosa yote yanayojitokeza,” amesema.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kurugongo, Edson Hanyuma amesema kuwa alipata wazo la ujenzi wa zahanati na kuwashirikisha viongozi wa kijiji ili waweze kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
“Wale wajumbe walikubali baadae tukaenda katika mkutano wa hadhara tukakubaliana hata kiasi cha mchango na wananchi wakalipokea vizuri wakaanza kufyatua matofali, kukusanya mawe na kutoa mchango wa shilingi elfu 10 kwa awamu ya kwanza na elfu 5 awamu ya pili…
Kwa michango yote ya awamu ya kwanza na ya pili ilikwenda vizuri mawe yalikusanywa lakini pia matofali yaliletwa eneo la mradi na ujenzi ukawa umeanza kwasababu pesa ya kumpa fundi ilikuwepo,” amesema.
Katika hatua nyingine Hanyuma amemshukuru Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) kwa ushirikiano mkubwa aliotoa hadi kuanza kwa ujenzi huo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.