Na Mwandishi Wetu
Halmshauri ya Wilaya Kasulu mkoani Kigoma siku ya kesho Alhamisi itazindua chanjo ya kitaifa ya ugonjwa wa Surua na Rubella ikipanga kuwachanja watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wapatao 106,410.
Hayo yamebainishwa wilayani Kasulu na Katibu Tawala wa Wilaya ya hiyo, Theresia Mtewele alipokuwa anafungua Kikao cha Kamati ya Afya Msingi (PHC) kilichohusisha wajumbe kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu na ile ya Mji hivi karibuni.
“Zoezi hili litachukua muda wa siku nne na litajumuisha watoa huduma watano kwa kila timu zitakazokuwa na watu wa kutoa chanjo, mtunza takwimu pamoja na muhamasishaji,” amesema.
Pia, amebainisha kuwa timu hizo zitapita sehemu za masoko, mashuleni, nyumba za ibada, vituo vya mabasi, kambi za wakimbizi na wavuvi na zile zinazohusisha mikusanyiko ya watoto.
“Nataadharisha usambazwaji wa taarifa potofu au zile za uchochezi zitakazosababisha wazazi kushindwa kuwapeleka watoto sehemu za kutolea chanjo.Nawaombeni muwasisitize sana wananchi kushiriki zoezi hili ili kufanikisha ufanisi wa kufikia viwango vya 100%,” amebainisha.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya Kasulu, Mageni Pondamali amesema kuwa chanjo hiyo itakuwa tofauti na ile ya Polio ambayo walipita nyumba kwa nyumba.
“Itakuwa ngumu kupita nyumba kwa nyumba kuchoma watoto sindano ndio maana tumeandaa vituo maalumu ili ikitokea shida tuweze kuikabili tofauti na ile ya Polio iliyokuwa inahusisha kudondoshea matone kwakuwa chanjo hii inahitaji umakini wa hali ya juu kidogo,” amesema.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.