Na Mwandishi Wetu
Bondi ya Miundombinu ya Samia itawasidia wakandarasi wazawa wanaotekeleza miradi yao chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) kulipwa fedha zao kwa wakati kitu kitakachopelekea miradi kukamilika katika muda uliopangwa.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Theresia Mtewele amebainisha hayo mapema hii leo wakati wa uzinduzi wa bondi hiyo wilayani humo tukio lililofanyika katika Tawi la Benki ya CRDB Wilaya ya Kasulu.
“Moja ya changamoto serikali ilikuwa inapitia ni wakandarasi kulipwa kwa wakati na kushindwa kumaliza miradi kwa wakati, bondi hii inaenda kuwa suluhisho kwa wenzetu na sisi wasimamizi wa miradi ya maendeleo kutupa unafuu kwasababu tutaenda kuisimamia kwa urahisi ukamilikaji wake ili wananchi waweze kuneemeka,” amesema.
Aidha, Theresia ameitaka benki hiyo kuhakikisha inatoa elimu kwa wananchi kwenye suala zima la uwekezaji kuhusiana na bondi hiyo kutokana na ufahamu wa masuala hayo kuwa chini ili lengo walilopanga la kuwakwamua watanzania kiuchumi liweze kufikiwa.
Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Kasulu, Erick Tesha amesema kuwa kupitia bondi hiyo mwekezaji atapata fursa ya kulipwa mpaka awamu nne kwa mwaka kwa kila robo inayohusisha miezi mitatu kupata malipo mara moja.
“Samia Bond inawekezwa kwa muda wa miaka mitano na katika miaka hiyo inapata riba ya 12% kwa mwaka… dirisha la ununuzi wa hati fungani hii limeanza jana na litafungwa Januari 17,2025, dirisha limefunguliwa kwa wawekezaji wote wenye kiwango cha kuanzia shilingi 500,00 na kuendelea,” amesema Tesha.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.