Na Mwandishi Wetu
Halamshauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma jana Jumanne Septemba 10,2024 imetekeleza mpango wa kuhama kutoka katika uendeshaji wa vikao vya mabaraza ya madiwani kwa kutumia makabrasha na kuanza kutumia vishikwambi.
Ambapo jumla ya vishikwambi 70 vimenunuliwa na kugawiwa kwa waheshimiwa madiwani,Kamati ya Uinzi na Usalama ya Wilaya ya Kasulu,wakuu wa divisheni na vitengo pamoja na baadhi ya viongozi Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo.
Akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Madiwani kujadili taarifa za Robo ya Nne ya mwaka 2023/2024 Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mhe. Eliya Kagoma amesema kuwa vifaa hivyo vitaleta matokeo chanya kwa kurahisisha upatikanaji wa taarifa pamoja na kuokoa fedha zilizokuwa zinatumika kwenye uandaaji wa makabrasha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Dkt. Semistatus H. Mashimba amesema kuwa ugawaji wa vishikwambi hivyo ni katika kuhakikisha utekelezaji wa shughuli za kiserikali zinafanywa kisasa zaidi ili kuwa na halmashauri endelevu inayobadilika kutokana na wakati.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kasulu, Mbelwa Chidebwe amesema jiografia ya halmshauri hiyo ina eneo kubwa la kiutawala hivyo ununuzi wa vishikwambi utapunguza gharama za uendeshaji na fedha zilizokuwa zinatumika kuandaa makabrasha zitakwenda kusaidia uetekelezaji miradi mingine ya maendeleo.
Diwani wa Viti Maalum kutoka Kata ya Nyamidaho, Mhe. Agness Kanyamangenge ameipongeza Kamati ya Fedha ya baraza hilo kwa kulipitisha jambo ambalo ni zuri litakalopunguza adha kwa wakuu wa divisheni na vitengo kusambaza makabrasha kwa madiwani ambapo kutokana na eneo la kijiografia kuwa kubwa fedha nyingi zilikuwa zinatumika.
Awali akizungumza katika tukio hilo Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu,Theresia Mtewele aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu amehimiza suala la umoja na mshikamano nchi inapoelekea katika uchaguzi pasipo kujali itikadi za kisiasa ili kutimiza azma ya serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.