Na Mwandishi Wetu
Watendaji wa Kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wamehimizwa kuwaelimisha wananchi kuhusiana na sheria ndogo ya kudhibiti Sumukuvu kwanini imeletwa ili itakapoanza kutumika isilete mgongano baina yao.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Theresia Mtewele ametoa wito huo leo Jumanne Julai 2,2024 wilayani humo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu kwenye warsha ya Mradi wa Tanpac ya Uwasilishaji wa Sheria Ndogo za Kudhibiti Sumukuvu.
Vilevile, amewataka watendaji hao kutilia mkazo suala la udhibiti wa sumu hiyo kutokana na Wilaya ya Kasulu mazao yake kulisha nchi zipatazo sita ili isitokee siku yakarudishwa mipakani kutokana na kuwa na viashiria hivyo na kuchafua taswira ya taifa.
Afisa Kilimo Mkuu kutoka Wizara ya Kilimo, Ntirankiza Misibo amesema kuwa sheria ndogo hizo kama zitasimamiwa vizuri zitaimarisha usalama wa chakula,kipato kuongezeka kwa wakulima kwakuwa mazao yao yatakuwa katika ubora mkubwa pamoja na afya za walaji kuimarika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Dkt. Semistatus H. Mashimba amesema kuwa sheria hizo hazijatungwa ili kufanya tatizo la Sumukuvu liendelee na kuwataka watendaji wa Divisheni ya Kilimo kutafuta njia nyingine ya namna ya kulimaliza.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Kitengo cha Sheria Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Emmanuel Ladislaus amesema kuwa halmshauri ina wajibu wa kuhimiza wakulima kufuata kanuni bora za kilimo kwenye utayarishaji wa mashamba, uvunaji na utunzaji wa mazao ili kudhibiti tatizo la Sumukuvu linaloathiri afya ya binadamu.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.