Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Balozi Simon Sirro, amezitaka halmashauri zote zilizopo katika Wilaya ya Kasulu kuhakikisha zinatenga maeneo mahususi kwa ajili ya uwekezaji, ili kuwawezesha kupata maeneo kwa urahisi bila vikwazo.
Balozi Sirro ametoa wito huo leo Jumanne, Julai 8, 2025, wakati wa ziara yake ya kujitambulisha kwa viongozi wa Serikali, watumishi, wananchi, viongozi wa dini na wazee maarufu, iliyofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu.
“Nafahamu wilaya yetu ina fursa nyingi za uwekezaji kupitia kilimo cha mazao ya chakula na biashara, pamoja na utalii. Nisisitize tu watendaji kuongeza ubunifu na kuweka mifumo mizuri ya usimamizi, sambamba na kutoa ushirikiano kwa wawekezaji waliopo na watakaoingia ili kuongeza pato la wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla,” amesema.
Aidha, kutokana na mkoa huo kupakana na baadhi ya nchi zenye changamoto za kiusalama, Balozi Sirro amehimiza watumishi wa umma kutoa elimu ya uraia kwa wananchi ili kuhakikisha wageni wanaoingia nchini wanazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo kwa lengo la kudumisha amani na utulivu.
Katika hotuba yake, amesisitiza umuhimu wa watendaji kuzingatia vipaumbele vya mkoa, ikiwemo usimamizi wa miradi ya maendeleo, utekelezaji wa sera ya matumizi bora ya ardhi, kukuza biashara na uwekezaji, kuibua vyanzo vipya vya mapato, pamoja na kuboresha huduma za elimu, afya na maji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu, amesema kuwa hali ya usalama katika wilaya hiyo ni shwari, na kwamba maeneo ambayo tayari yamechukuliwa na wawekezaji wakubwa yatalindwa kwa gharama yoyote ili kuendeleza hamasa ya uwekezaji zaidi.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, akizungumza kwa niaba ya wananchi, amesema kuwa wao kama wawakilishi wa majimbo ya Kasulu wanajivunia mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala, ambayo imeleta maendeleo makubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.