Na Mwandishi Wetu.
Walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kutia juhudi kwenye kuielewa mifumo mbalimbali ya kidigitali ya serikali wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku kwenye vituo vyao vya kazi.
Afisa Elimu Mkoa wa Kigoma, Paulina Ndigeza ameyabainisha hayo wilayani humo jana kwenye hafla ya Siku Maalumu ya Elimu kwa Mwaka 2024 iliyojikita kutoa tuzo kwa walimu na shule mbalimbali zilizofanya vizuri katika mitihani mbalimbali ya kitaifa ya upimaji kwa mwaka 2023.
“Kila mmoja lazima ajifunze mifumo kwakuwa mambo ya kiutumishi kama OPRAS yapo kwenye mfumo ndio maana watumishi wote tunatakiwa kujisajili, kwahiyo vigezo vyote vya utendaji kazi vilivyokuwa vinatumia karatasi sasa hivi mambo hayo hakuna na huo ni mfumo wa nchi nzima,” amesema.
Pia, ameshauri ushirikishwaji wa jamii katika suala la kudhibiti utoro ili kuongeza kiwango cha ufaulu.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Emmanuel Ladislaus amesema kuwa kikao hicho kimefanyika ili kufanya tathimini ya kina itakayofanya maboresho kutoka mahali walipokuwa na kusonga mbele kwenye suala la taaluma.
“Katika halmshauri yetu tunajivunia kufanya vizuri na hilo tumelifanya kwa vitendo pamoja na jiografia yetu amabayo huwezi kuichora kwa urahisi lakini tumeweza kutumia rasilimali ndogo tulizokuwa nazo kufanya mambo makubwa kwenye suala la taaluma kwa mwaka uliopita.
Afisa Elimu Sekondari Taaluma, Mussa Kanyoe akitoa taarifa ya sekta ya elimu kwa mwaka uliopita amebainisha kuwa kumekuwa na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya awali kutoka 97% mwaka 2022 kufikia 105% kwa mwaka 2023.
“Kwa Darasa la Kwanza tumetoka 105% mwaka 2022 hadi 109% kwa mwaka 2023, mafanikio haya yametokana na utekelezaji wa elimu bila malipo ulioanza Januari mwaka 2016,” amesema.
Kwa upande wake Afisa Elimu Awali na Msingi wa Halmshauri hiyo, Elestina Chanafi amesema kuwa wanatambua jitihada zilizofanywa na wadau mbalimbali wa sekta hiyo kitu kilicholeta mabadiliko chanya kwenye suala la ufundishaji na kuongeza ufaulu.
“Tulitamani kuwa na siku hii maalumu kama kisababisho cha mafanikio haya ya kielimu ili tuambiane asante pamoja na kupongezana ikiwemo kuweka mikakati ya kuwa bora zaidi ya hivi tulivyokuwa leo,” amebainisha.
Katika hatua nyingine mwakilishi wa Mwenyekiti wa halmshauri hiyo, Laurent Poteza alishauri kwa mwaka unaofuata kuwajumisha wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani mbalimbali ya upimaji kitaifa ili kuwatia hamasa.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.