Shule za msingi katika halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, zitanufaika na mpango wa lishe shuleni unaofadhiliwa na shirika la chakula duniani WFP, anaripoti Respice Swetu.
Hayo yamebainika kufuatia shirika hilo kuanza utekelezaji wa mpango huo kwa kugawa mbegu za mahindi, maharage, mchicha na miche ya parachichi kwa shule 15 za msingi zitakazoanza kunufaika na mpango huo.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa usambazaji wa mbegu na miche hiyo, Ofisa elimu watu wazima halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Simon Kichumu, amezitaja shule zilizopelekewa mbegu hizo kuwa ni Nyakatoke, Nyachenda, Nyakelela, Kasasa, Muungano, Nyarugusu, Nyamuganza na Kumkambati.
Sambamba na hizo, shule nyingine zilizomo katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo kuwa ni Heru Ushingo, Kigadye, Nyamiyaga, Asante Nyerere, Nkundusi, Rusesa na Kakirungu.
"Kwa kuwa kila shule itatakiwa kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wake kutokana na nafaka zitakazozalishwa kupitia mpango huo, kilo 40 za mbegu ya maharage, kilo 8 za mbegu ya mahindi, miche 10 ya parachichi na mbegu za mboga mboga zimetolewa kwa shule hizo", amesema.
Ameongeza kuwa, mpango huo unaotekelezwa na WFP kwa kushirikiana na kituo cha utafiti wa mbegu TARI cha jijini Arusha, unatarajiwa kuzaa matunda kutokana utayari uliooneshwa na shule hizo wakati wa kupokea mbegu hizo.
Mpango huo unaotekelezwa katika halmashauri tatu za mkoa wa Kigoma, umeanza kwa kuzifikia shule zilizo na maeneo ya kulima yenye ukubwa wa heka mbili na nusu na kuendelea.
Pamoja na halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, halmashauri nyingine zitakazonufaka na mpango huo katika mkoa wa Kigoma ni Kasulu Mji na halmashauri ya Wilaya ya Kibondo.
Kufanikiwa kwa mpango huo, kutasadifu msemo wa wahenga wa kumpa mtu nyavu badala ya samaki waliovuliwa.
Pichani, walimu na wajumbe wa kamati ya shule ya msingi Nyakelela walipokuwa wakipokea mbegu za maharage, mahindi na miche ya miti ya parachichi kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.