Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawaandikisha watoto waliofikisha umri wa kuanza darasa la awali na la kwanza kwa mwaka wa masomo 2024.
Mwakisu ameyasema hayo hivi karibuni kwenye ziara ya siku mbili ya Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kasulu kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho.
Amesema miradi ya Boost iliyobuniwa kwa ajili ya shule za msingi tayari imekamilika ili ifikapo Januari mwakani watoto waweze kuingia na hakuna kikwazo chochote kinachoweza kukwamisha.
“Wananchi wasije wakaficha watoto kwa shughuli zao binafsi hasa za kuchunga Ng’ombe na kuacha kuwapeleka shule tutawafuatilia wale wote watakaoficha watoto wasiende shule… kama ni chekechea aende kwakuwa shule zao zipo na nina uhakika wakifika pale hawatakata tamaa kwasabau kuna michezo mingi,” amesema.
Katika hatua nyingine Mwakisu aliwahimiza wananchi kuibua miradi ya maendeleo na kuitekeleza kwa nguvu zao katika hatua za awali ili baadae inapofikia hatua nzuri serikali iweze kusaidia.
“Hiyo ndio sera ya nchi kwamba wananchi wakichangia baadae serikali inakuja kutoa fedha kwa ajili ya ukamilishaji… wito wangu waendelee kujitolea kwa kujenga miundombinu tofauti ikishafika hatua ya boma sisi serikali tunakuja kuichukua ili kuleta tija kwa kile wananchi walichokikusudia,” amesema.
Katika ziara hiyo kamati hiyo ilipata fursa ya kutembelea shule ya msingi ya mchepuo wa kiingereza ya ‘Hope Pre and Primary’ iliyopo Kata ya Muzye inayomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu na kupongeza namna ilivyokuwa na mazingira wezeshi ya kuwafundishia watoto.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.