Wakati zoezi la utoaji wa chanjo ya matone kuzuwia maambukizi ya ugonjwa wa polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano likiwa linaendelea, jumla ya watoto elfu sabini na saba na mia nne kumi na tano katika halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wamepewa chanjo hiyo.
Hayo yamebainika wakati wa uzinduzi wa zoezi la utoaji wa chanjo hiyo lililofanyika kwenye kituo cha afya cha Nyakitonto.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Katibu wa afya wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Joseph Mwanambesi amesema, zoezi hilo linalofanyika kwa kampeni ya nyumba kwa nyumba linakwenda vizuri na kuleta matumaini ya kuwafikia watoto wote wenye umri huo.
Aliongeza kuwa, halmashauri ya Wilaya ya Kasulu iliyolenga kutoa chanjo kwa watoto laki moja arobaini na saba na mia moja ishirini na nne, imekwishatoa chanjo hiyo kwa watoto sabini na saba elfu mia nne kumi na tano huku muda uliopangwa kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi hilo ukiwa haujaisha.
Kwa upande wake, afisaelimu msingi wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Elnesta Chanafi, amewataka wazazi na walezi katika halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, kuwapeleka watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano kwenye vituo vya afya na kuwatoa pindi watoa chanjo wanapofika kwenye makazi yao.
Chanafi aliyemwakikisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kuzindua utoaji wa chanjo hiyo, ameyataja baadhi ya madhara yatokanayo na ugonjwa wa polio kuwa ni pamoja na mtoto kupooza hali inayopelekea kupata ulemavu.
Madhara mengine kwa mujibu wa Chanafi ni adha watakayoipata wazazi ya kutumia muda mwingi katika kuwahudumia watoto watakaokuwa na ulemavu utakaotokana na ugonjwa huo.
Pichani: Kaimu mganga mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Amani Mkemwa (mwenye shati la drafti) na Afisaelimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya kasulu Elnesta Chanafi wakati wa uzinduzi wa chanjo hiyo.
Wazazi wakiwa kwenye kituo cha afya cha Nyakitonto walipowapeleka watoto wao kupata chanjo ya kuzuwia maambukizi ya ugonjwa wa polio Alhamisia Mei 19, mwaka huu(2022).
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.