Na Mwandishi Wetu
Wenyeviti wa vijiji, watendaji wa kata pamoja na viongozi wa dini katika Halamshauri ya Wilaya ya Kasulu wametakiwa kuhimiza wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto kijunga na kidato cha kwanza.
Hayo yamebainishwa mapema hii leo wilayani humo na Afisa Elimu Taaluma (Sekondari) wa halmashauri hiyo, Mussa Kanyoe alipopita kukagua mapokezi ya wanafunzi hao na kubainisha kuwa wanafunzi wote watapokelewa hata kama hawajakamilisha baadhi ya vitu na maandalizi mengine yatafanyika wakiwa tayari shuleni.
“Lengo ni watoto wafike mapema na kuanza kujifunza kwa pamoja na si kufika taratibu kwasababu kuchelewa kufika shuleni kutasababisha watoto wengine wasiwe vizuri kitaaluma,” amesema.
Amesema ataendelea kupita mashuleni kuhakikisha wale wote waliopata nafasi wanaanza masomo huku akifuraishwa kwenye baadhi ya shule alizopita kwa namna wazazi walivyoandamana na watoto kwenda kuwasajili.
Afisa Elimu Kata ya Titye, Yoab Henyura amebainisha kuwa watahakikisha wanatoa matangazo kwa kupita kila kijiji ili wazazi waweze kuleta watoto wajiunge na kidato hicho.
“Mtoto aletwe shuleni vyovyote vile atakavyokuwa kama hana sare au mkoba anatakiwa aje shule ili aanze masomo hivyo vitu vingine makubaliano yetu ni kwamba mzazi ataendelea kutafuta polepole,” amesema.
Mmoja wa wazazi aliyemleta mwanaye katika Shule ya Sekondari ya Nkundusi,Fadhila Kabuyanga aliishukuru serikali kwa namna ilivyofanya maandalizi mazuri ya kuwapokea watoto na kuwataka wazazi wengine kuhakikisha wanawapeleka watoto kupata elimu.
Naye Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Rungwe Mpya, Elton Ntazina amesema kuwa waraka wa serikali umeainisha mwanafunzi kuanza masomo bila masharti yeyote na wako tayari kuwapokea ili lengo hilo lipate kutimia.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.