Na Mwandishi Wetu
Tafiti iliyofanyika katika Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imebaini kilimo cha zao la Uyoga kitawanufaisha wananchi wa eneo husika kwakuwa uhitaji wake ni mkubwa katika soko.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Mkufunzi Mwandamizi kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Halima Kazindolo kwenye warsha ya wadau kuhusu tathimini ya mradi wa uzalishaji wa Uyoga katika wilaya hiyo.
Amesema kabla ya kuanza utekelezaji wa kilimo hicho ni lazima hamasa itolewe kwa wakulima kuwa kuna uhakika wa soko pamoja na kuchukua muda mfupi wa hadi kukamilika kwake.
“Uyoga ni zao linalokaa kwa muda mfupi sisi wataalamu tunaweza kusema ni namna gani tunaweza kuliongezea uhai ili liweze kufika katika masoko mengine ambapo huko kilo moja bei inaanzia shilingi elfu nane hadi ishirini,” amesema.
Pia, amebainisha kuwa tafiti hiyo imebaini zao hilo linapendwa na watu wapo tayari kulilima, kitu kitakachosaidia upatikanaji wake na kuachana na ule wa kienyeji ambao kutokana na changamoto ya misitu kuwa kubwa upatikanaji wake umekuwa shida.
Naye Andrew Ching’ole kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) amesema kuwa kupitia tathimini hiyo amejifunza Uyoga unalimika kipindi chote cha mwaka na kukamilika ndani ya miezi miwili kabla ya kufika sokoni.
“Nimejifunza Uyoga una faida katika masuala ya lishe kwa kuwa na vitamini nyingi kwa pamoja, madini mengi, kuimarisha ngozi, kutibu kisukari, moyo, shinikizo la damu na figo magonjwa ambayo yanatusumbua sana,” amesema.
Meneja wa SIDO Mkoa wa Kigoma, Gervas Ntahamba amebainisha kuwa tafiti hiyo imefanyika katika vijiji vinne katika wilaya hiyo na kutoka na taarifa ambayo haijakamilika hivyo kupitia uwasilishaji huo watapata maoni na mawazo kwa ajili ya maboresho.
Awali akifungua uwasilishaji huo mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Kasulu,Audax Kamugisha aliwataka washiriki kuisikiliza kwa makini tathimini hiyo ili kubaini kama imefikia malengo yaliyokusudiwa.
“Kilimo cha Uyoga ni kikubwa na chenye manufaa kwa jamii kwenye kuwaingizia pesa ila kama hujaelezwa huwezi kujua undani wake lakini tukiielewa tathimini wenzetu waliofanya tunaweza kuingia katika kilimo hiki vizuri,”amesema.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.