Shirika la umoja wa mataifa la kuwasaidia wakimbizi duniani UNHCR, limetoa msaada wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mia moja kwa wakazi wa kijiji cha Kagerankanda wilayani Kasulu kwa kujenga vyumba viwili vya madarasa, choo chenye matundu sita na kuweka mfumo wa maji, anaripoti Respice Swetu
Akitoa taarifa ya ujenzi wakati wa hafla ya kukabidhi miundombinu hiyo, mhandisi wa shirika la UNHCR aliyesimama kazi hiyo Simon Peche ameeleza kuwa jumla ya shilingi milioni mia moja kumi na mbili, laki tano na ishirini na nane elfu zimetumika.
Peche aliyekuwa ameambatana na maafisa wengine wa shirika hilo wakati wa makabidhiano hayo amesema kuwa, UNHCR kupitia mpango wa kusaidia maeneo yaliyoathiriwa na wakimbizi, wataendelea kusaidia maeneo hayo kadri itakavyowezekana.
Ameongeza kuwa msaada kama huo ulioambatana na uwekaji wa madawati kwenye vyumba hivyo, umefanyika pia katika halmashauri za wilaya ya Kibondo na Kakonko mkoani Kigoma.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya Katibu Tawala wa mkoa wa Kigoma, Ofisaelimu taaluma wa mkoa huo Joas Jonas amelishukuru shirika hilo na kuwataka wakazi wa Kagerankanda kuyatunza majengo hayo.
"Pamoja na kuyatunza mnatakiwa kuweka utaratibu wa kuanza kuyatumia mara shule zitakapofunguliwa Januari mwaka kesho", aliagiza.
Miundombinu hiyo iliyojengwa kwenye eneo la shule ya msingi ya Nyanzaza iliyoanzishwa zaidi ya miaka kumi iliyopita, inakusudiwa kupunguza msongamano wa wanafunzi kwenye shule mama ya Kagerankanda uliotokana na kukosekana kwa madarasa kwenye eneo la shule ya msingi ya Nyanzaza.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ofisaelimu wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Elestina Chanafi amesema, kupatikana kwa miundombinu hiyo kutaendeleza ufaulu wa shule hiyo ambayo katika matokeo ya mtihani wa kuhitimu darasa la saba uliofanyika mwaka jana, imefaulisha kwa zaidi ya asilimia 90.
Msaada huo ni mwendelezo wa shirika hilo kuishika mkono halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ambapo katika siku za karibuni shirika hilo, limeikabidhi halmashauri ya Wilaya ya Kasulu matundu sita ya vyoo vilivyojengwa kwenye shule ya msingi ya Kumtundu.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.