Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Joseph Kashushura amesema ukodishaji wa pango la ardhi katika Shamba la Makere Kusini umesaidia halmashauri kukusanya mapato ya kutosha kitu kilichopelekea kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.
Kashushura amebainisha hayo leo Ijumaa katika Kijiji cha Mvugwe wilayani humo wakati wa ziara ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda aliposimama eneo hilo kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.
Amesema kupitia mapato hayo yaliyokusanywa halmashauri imefanikiwa kutekeleza ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Kitanga,kusaidia vikundi mbalimbali vya wanawake pamoja na ujenzi wa shule ya kisasa ya mchepuo wa kiingereza ya ‘Hope Pre and Primary.
Akizungumza katika tukio hilo Makonda amewaelimisha wananchi kuwa halmashauri inapata kujiendesha kupitia fedha kutoka serikali kuu pamoja na ukusanyaji wa mapato ya ndani kama wanavyofanya katika shamba hilo la Makere Kusini.
“Niagize kamati ya siasa ya mkoa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa iunde tume kuchunguza matumizi ya fedha ya shamba hilo si jambo la tamko lazima tuangalie faida zitokanazo na shamba hilo…naomba timu ipitie makubaliano ili kata zilizoathiriwa na hilo shamba zipewe kipaumbele katika suala la maendeleo,” amebainisha.
Aidha, amewataka wenyeviti wa vijiji na vitongoji katika halmashauri hiyo kutambua wakulima waliopo katika maeneo yao ili kuwabaini wale wasiokuwa waaminifu katika mchakato wa kukusanya ushuru wa mazao.
“Hata tukienda kwenye shamba kuna wasio waaminifu kila kiongozi katika eneo lake anajua wakulima wake wanaolima hivyo shangwe zenu zisinifanye nisisimamie ukweli ambao mimi ni muumini wake,” ameongeza Makonda.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.