Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kasulu akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Kigadye(hawapo pichani) wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Wilaya iliyofanyika kwa lengo la kufahamu hali halisi ya ushirikishwaji wa wananchi katika utoaji wa maeneo ya vijiji kwa Halmashauri kwa lengo la kumkodisha maeneo hayo Mwekezaji Kigoma Sugar.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Simon Anange akizungumza na Wananchi (Hawapo pichani) akiwa pamoja na Viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi, Wah. madiwani na wataalam walioshiriki ziara ya Kamati ya Siasa iliyofanyika Leo Tarehe 29.5.2019.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nyarugusu waliojitokeza kukutana na kamati ya Siasa ya Wilaya.
Na. Andrew Ginnethon-Kasulu.
Wakazi wa vijiji vya Kiyungwe, Nyarugusu, na Kigadye wamethibitisha taratibu zilifuatwa wakati wa utoaji wa baadhi ya maeneokatika vijiji hivyo ili kuipa Halmashauri ambayo ipo kwenye mchakato wa kumkodishia Mwekezaji M/S Kigoma Sugar Company Ltd kwa ajili ya uwekezaji wa Kiwanda cha Sukari.
Hayo yamebainika leo tarehe 29.5.2019 wakati kamati ya Siasa Wilaya ya Kasulu ilipofanya ziara na kuongea na wananchi kwenye vijiji hivyo, kwa kushirikiana na Wajumbe wa Kamati ya Fedha pamoja na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.
Kamati hiyo imewahoji baadhi ya wananchi waliokua wajumbe wa mabaraza ya Ardhi pamoja na viongozi mbalimbali waliowahi kushika nyadhifa kwenye vijiji hivyo, ambapo wamethibitisha kuwa taratibu zote ikiwemo Mikutano ya vijiji na ushirikishwaji wa kila hatua vilifanyika.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kan. Simon Anange, amewasisitiza wakazi wa vijiji hivyo kuwa wawazi mbele ya Kamati, kuhusu suala zima la utoaji wa Maeneo hayo kwa Halmashauri kwa Lengo la uwekezaji. “Tumekuja ili kamati ya Siasa ya wilaya, ijiridhishe kuhusu taratibu zilizotumika katika upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji ya Kigoma Sugar”
Amewataka wananchi hao kuyapuuza maneno ya upotoshaji yanayoenezwa na baadhi ya wananchi kuwa maeneo hayo yana mgogoro huku wakiwa na lengo la kuchelewesha au kuzuia uwekezaji kwa manufaa yao binafsi ikiwemo ufugaji usiofuata utaratibu.
Kan. Anange amesema uwepo wa Kiwanda hicho cha Sukari utasaidia kupatikana kwa ajira za kudumu zaidi ya 600 na amewataka wakazi hao waachane na utaratibu wa kuuza ardhi bila sababu za msingi.
Akitoa ufafanuzi kwa Wajumbe wa kamati ya siasa wilaya, Mkurugenzi Mtendaji Mha. Godfrey Kasekenya, amesema wananchi watapata fursa ya kulima miwa na kupatiwa Pembejeo na Mwekezaji kisha watarejesha gharama wakati wa mauzo.
Amesema kuwa, eneo hilo halina mgogoro kwa sababu wakazi wachache waliokuwa wakiishi kinyume na utaratibu, walishatengewa eneo lenye zaidi ya Hekta 1000 katika kitongoji cha Mkuyuni kilichopo kata ya Nyamidaho.
Mwenyekiti wa CCM wilaya, Ngd Mbelwa Abdallah, amepongeza utaratibu wa ushirikishwaji uliofanyanyika ambapo umepelekea Kamati ya siasa kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu masuala ya kiutekelezaji Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
“Utaratibu huu unapelekea kuondoa shaka na kupata nafasi ya Chama cha Mapinduzi ambacho ndicho chenye dhamana ya kuongoza Nchi, kuona na kushauri juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Tumejiridhisha kuwa taratibu za upatikanaji maeneo zimefuatwa na sisi kama Chama tumebariki taratibu zinazofuata ziendelee” amehitimisha Mbelwa.
Ndg. Riziki Gervas ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyarugusu, amesema mikutano mbalimbali ya kisheria ilifanyika na wananchi walishirikishwa kila hatua, Muhtasari uliandikwa na wananchi wanao uelewa wa kutosha kuhusu suala la mwekezaji.
Ziara hiyo imehitimishwa kwa kamati kutembelea Kituo cha Afya Nyamidaho pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Kasulu. Katika kituo cha afya Nyamidaho, kamati imekagua na kushuhudia utekelezaji ma maagizo ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge 2019 Ndg. Mzee Mkongea Ali, aliyeagiza kufanyika marekebisho kadhaa kwenye majengo ya Kituo cha Afya Nyamidaho. Kamati imekagua na kuridhika na marekebisho yaliyofanyika kisha kutoa pongezi kwa uongozi wa Halmashauri kwa utekelezaji.
Ikiwa kwenye Mradi wa ujenzi wa Hospitali ya wilaya, kamati imekagua na kuona maendeleo ya ujenzi wa majengo mbalimbali na kutoa ushauri juu ya masula kadhaa ya kiutendaji.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.