Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, imeanza kutekeleza ujenzi wa vyumba 41 vya madarasa ya shule za sekondari baada ya kupokea shilingi milioni 820 kwa ajili ya ujenzi huo, anaripoti Respice Swetu.
Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu ametoa taarifa hiyo alipokuwa akizungumza na baraza la madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu katika ukumbi wa halmashauri hiyo hivi karibuni.
Amesema kuwa mara baada ya kufika kwa pesa hizo, halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ilianza utekelezaji wa ujenzi huo ambapo mpaka sasa, hatua mbalimbali za ujenzi zimefikiwa.
"Nimezunguka shule zote kuona kazi inavyokwenda, maeneo mengi yapo kwenye msingi na wengine wameanza kupandisha ukuta, changamoto iliyopo ni upungufu wa saruji," alisema.
Kufuatia upungufu huo, Kanali Mwakisu ameielekeza halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kuagiza saruji moja kwa moja kutoka kiwandani.
Mwakisu ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya usalama ya wilaya, amekitumia kikao hicho pia kuwashukuru wakazi wa wilaya ya Kasulu kwa ushirikiano wanaompatia katika kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na yale ya kitaifa.
"Nachukua nafasi hii kuwashukuruni sana wananchi wote wa wilaya ya Kasulu kwa ushirikiano mkubwa mnaonipa, na hata siku nitakapoondoka Kasulu nitakuwa nawakumbuka, kwa hakika mmeniheshimisha," alisema.
Mwakisu aliyataja matukio aliyopewa ushirikiano mkubwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa ya uviko, sensa ya watu na makazi, mbio za mwenge wa Uhuru na ugeni wa mheshimiwa Rais Samia Suluhu alipoitembelea wilaya ya Kasulu Oktoba mwaka huu.
Hatua ya ujenzi iliyofikiwa, vyumba vya madarasa shule ya Sekondari Kimenyi.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.