Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu amesema kuwa Tanzania inakabiliwa na tatizo la uharibifu wa mazingira ikiwemo upotevu wa hekta 4600 za misitu kwa mwaka ndio maana serikali imeeandaa mikakati na sera zingine za kukuza uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
Kanali Mwakisu ameyabainisha hayo leo Jumanne Juni 5, 2024 wilayani humo kwenye maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kiwilaya yalifanyika katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu.
Ambapo amesema kuwa tokea Januari 31, 2024 serikali imetoa katazo kwa taasisi za umma zinazopika chakula cha watu zaidi ya 100 kuacha matumizi ya kuni na badala yake zitumie nishati mbadala ili kusaidia utunzaji wa mazingira.
Aidha,amehimiza jamii ya wakimbizi kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa eneo hilo na serikali, mashirika yote yanayohudumia wakimbizi na wadau wa masuala ya kibinadamu kwa kupanda miti na kutunza vyanzo vya maji vinavyohitaji upandwaji wa miti rafiki inayosaidia ustawi wake.
Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) wilayani Kasulu, Jean Ngomoni amesema kuwa changamoto kubwa iliyo mbele yao kwa mashirika yote yanayofanya kazi ndani ya kambi ni kuicha Nyarugusu ikiwa salama na mazingira yake yakiendelea kutunzwa.
“Serikali inashirikiana na sisi na wenyeji wako tayari kutusaidia pamoja na wakimbizi kuhakikisha Nyarugusu tunaicha salama tunashirikiana nao pamoja na wadau wengine wa maendeleo ambao wapo tayari kutusaidia zikiwemo nchi ya Ubelgiji na Uswidi,” amesema.
Kaimu Mkuu wa Kambi hiyo, Humphrey Mrema amelishukuru Shirika la UNHCR kwa kazi kubwa wanayoifanya kambini humo kwa kuhakikisha mazingira yake yanakuwa salama kutokana na uwepo wa wakimbizi kuchangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Theresia Mtewele amebainisha kuwa mikakati inayofanywa na mashirika mbalimbali kambini humo imesaidia utunzaji wa mazingira kwa kuhamsisha utumiaji wa nishati safi na mbadala za kupikia tofauti na kuni na mkaa.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.