Naibu Katibu Mkuu. Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dk. Michael Francisakifafanua jambo kwa Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya na Mji wa Kasulu(hawapo pichani)
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mha.Godfrey Kasekenya (wa kwanza kulia) akisikiliza swali kutoka kwa Mtumishi(hayupo pichani) wakati Naibu Katibu Mkuu Utumushi wa Umma aliporuhusu watumishi wa Wilaya ya Kasulu kuuliza maswali mbalimbali na kueleza changamoto zao.
Baadhi ya wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na watumishi wa Wilaya ya Kasulu kutoka Kada mbalimbali wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma Dk. Michael Francis wakati akiongea nao, mapema leo katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Kasulu.
Naibu Katibu Mkuu. Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dk. Michael Francis amekutana na kuzungumza, kushauri kisha kutoa utatuzi wa Changamoto zinazowakabili watumishi wa kada mbalimbali katika Wilaya ya Kasulu.
Dk. Francis amekutana na watumishi hao leo tarehe 22.8.2019 katika Ukumbi wa chuo cha ualimu Kasulu, ambapo amewakumbusha wajibu wa Utumishi wa Umma ikiwemo utendaji kazi kwa weledi, heshima kazini, kuboresha na kudumisha uwajibikaji ili kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli katika kuliendeleza Taifa.
Dk. Francis ametolea ufafanuzi kuhusu changamoto mbalimbali za kiutumishi ikiwemo malimbikizo ya Mishahara pamoja na madai mbalimbali ambapo alifafanua kuwa, Serikali imekuwa ikiendelea kulipa madeni hayo baada ya kuyahakiki kutokana na baadhi yake kutokuwa na uhalali na kukidhi vigezo.
Amewataka wanaohusika na kusimamia masuala ya ajira, kutenda haki kwa kuzingatia kanuni, Sheria na miongozo badala ya kutanguliza undugu, ujamaa, ukabila, Imani za kidini au namna yoyote ya Mahusiano katika utoaji wa ajira hizo.
Akipokea changamoto mbalimbali za watumishi, Dk. Francis amewaasa maafisa Utumishi kujenga mahuziano mazuri na watumishi wa kada mbalimbali wanaowasimamia hali itakayopelekea kuyafurahia mazingira ya kazi na kuwepo kwa utulivu.
Akiwasilisha changamoto zinazoukabili Mkoa wa Kigoma, Kaimu Katibu Tawala Mkoa Ndg. Daniel Machunda, amezitaja kuwa ni upungufu wa Watumishi wa Umma, uhaba wa Nyumba za watumishi, uwepo wa Madai ya stahiki mbalimbali za watumishi, kuchelewa kupandishwa vyeo, uwepo wa idadi kubwa ya watumishi wanaohama pamoja na baadhi ya wanaoajiriwa kushindwa kufika kwa sababu za usalama kutokana na Mkoa kupakana na Nchi ambazo hazina utulivu na Amani ya kudumu.
Ndg. Machunda ameyataja mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa kiutekelezaji chini ya Serikali ya Awamu ya Tano, ikiwemo ongezeko la nidhamu kwa watumishi, udhibiti wa Ajira hewa, uboreshwaji wa utoaji wa huduma kwa watumishi wa Umma, kuendelea kuimarika kwa Ikama ya watumishi na udhibiti wa madeni yasiyo ya lazima.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.