Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu(wa pili kulia) Mhandisi Godfrey Kasekenya akifurahia jambo wakati wa sherehe ya uwekaji jiwe la msingi katika kituo cha afya cha Nyamidaho. Kushoto kwake ni Mh. Said Ndiyunze Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Kasulu.
Mkurugenzi wa Hamlmashauri ya wilaya ya Kasulu Mhandisi Godfrey Kasekenya akipokea zawadi kutoka kwa watumishi wa Kituo cha Afya Nyamidaho katika kuonnyesha na kuthamini bidii pamoja na mchango wake katika kusimamia na kuhakikisha ujenzi wa Kituo cha Afya Nyamidaho unafanyika na kukamilika.
Na,Andrew Mlama.Kasulu.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganga, ameweka jiwe la msingi katika kituo cha Afya Nyamidaho ambacho hapo awali ilikua ni Zahanati kisha kupanuliwa na kupandishwa hadhi kuwa kituo cha Afya ambapo ujenzi wake umegharimu Sh. 5,37,800,000 ambapo sh. Mil 500 ni kutoka serikali kuu na kiasi kilichobaki ni nguvu za wananchi pamoja na mchango kutoka halmashauri.
Uwekaji huo wa jiwe la msingi umefanyika leo tarehe 11.08.2018 katika kata ya Nyamidaho iliyopo wilayani hapa, ambapo zimefanyika kazi za ujenzi wa miundombinu na majengo sita ikiwemo jengo la maabara, wodi ya wajawazito na watoto, jengo la upasuaji, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la wagonjwa wa nje na nyumba ya mganga.
Baada ya uwekaji jiwe la msingi ,amekagua majengo hayo ambayo ukamilifu wake umetimia kwa 98%, amesisitiza uwepo wa akina baba wakati wake zao wanapojifungua ili nao waweze kuhisi, kusikia na kuona uzito wa tendo la uzazi unaowakabaili wake zao. Amesisitiza watumishi na wananchi kuyatunza majengo hayo ili yaweze kudumu na ameridhishwa kwa kiasi kikubwa na ujenzi huo.
Katika hotuba yake baada ya uwekaji jiwe la msingi, mkuu wa mkoa wa Kigoma amewashukuru wananchi kwa kujitolea akiba ya Matofali 48,000, kuchimba mtaro na kuweka mabomba ili kuhakikisha kituo kinapata maji ya uhakika. “katika maendeleo hakuna Siasa , wananchi fanyeni maendeleo kwani utoaji na upatikanaji wa huduma haujali vyama” amesisitiza Maganga.
Amewataka wanajamii kuishi kwa kiasi ikiwemo kula, kunywa na kujenga tabia ya kuridhika pamoja na kufanya mazoezi ya mara kwa mara kwa lengo la kuimarisha Afya na kudumisha utimamu wa miili na kupelekea utendaji na utekelezaji mzuri wa majukumu ya kila siku kwa maendeleo yao.
Amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono Chama Cha Mapinduzi ili kuhakikisha sera zake zinatekelezwa. Aidha amewahakikishia kutekeleza maombi yote waliyo yatoa kwake awamu kwa awamu na ikiwemo uwekaji wa umeme katika kituo hicho cha Afya jambo ambalo amelikabidhi kwa mbunge wa Kasulu vijijini Mh. Augustino Vuma.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi, Mkurugenzi mtendaji wa Halmahsauri ya wilaya Kasulu Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema kuwa halmashauri imetenga zaidi y ash. Mil 5 kwa ajili ya ujenzi wa magati mawili eneo ambalo bomba la maji la kituo cha Afya limepita kwalengo la kutoa huduma ya maji safi kwa wananchi.
Aidha amemuomba mkuu wa mkoa asaidie kufikisha serikalini maombi ya kusaidiwa kufanikisha ujenzi wa nyumba za watumishi, ujenzi wa wodi ya wanawake, watoto na wanaume, jengo la kufulia nguo pamoja na kuweka msukumo ili kuweka umeme katika majengo na kupatikana kwa jenereta itakayotumika itakapotokea dharura ya kukatika kwa umeme.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Kasulu Bw. Mageni Pondamali amesema kuwa huduma zitakazotolewa katika kituo hicho ni pamoja na huduma ya upasuaji kwa akina mama wanaoshindwa kujifungua,upatikanaji vipimo vya msingi, kuhifadhi maiti na makazi bora kwa watumishi wa Afya. Amesema ujenzi umekamilika kwa 98%. Amesema mradi huo utakapokamilika utahudumia watu 1,76,212 wa tarafa ya Makere.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.