Zikiwa zimetimia siku tano tangu kuanza kwa mitihani ya kuhitimu kidato cha nne inayoendelea nchini pote, wakuu wa shule za Sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wameonesha matumaini makubwa kuwa vijana wao watafanya vizuri kwenye mitihani hiyo
Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa shule za Sekondari za Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ofisini kwake, mkuu wa shule ya Sekondari ya Rungwempya Dickson Nussu amesema kuwa, kutokana na maandalizi waliyoyafanya, wanayo matumaini makubwa kuwa vijana wao watafanya vizuri.
Amesema kuwa walimu wamewaandaa watahiniwa wao kikamilifu kukabiliana na mitihani hiyo hali inayowapa matumaini kuwa watashinda.
"Naamini vijana wetu watafanya vizuri na kupata ufaulu wa kuendelea na elimu ya juu pamoja na kujiunga na vyuo mbalimbali", amesema.
Kwa upande wake, ofisaelimu wa Sekondari katika Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Bahati Onesmo, amewataja watahiniwa wanaofanya mitihani hiyo kuwa ni 1813 kati yao wavulana wakiwa 1026 na wasichana 787.
Bahati ambaye pia ni katibu wa kamati ya mtihani ya wilaya ameongeza kwa kusema kuwa kati ya watahiniwa hao, watahiniwa 1809 ni wa shule huku watahiniwa 4 wakiwa ni watahiniwa binafsi.
"Hao watahiniwa wanne wapo kwenye kituo cha shule ya Sekondari ya Makere", amesema.
Kuhusu maendeleo ya ufanyikaji wa mitihani hiyo iliyosimama kupisha mapumziko ya mwisho wa wiki amesema, mpaka kufikia sasa, hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza.
"Mitihani inaendelea vizuri, hakuna changamoto yoyote katika vituo vyote vya mitihani mpaka sasa, na kwa maandalizi tuliyoyafanya naamini tutamaliza salama", amesema.
Ratiba ya baraza la mitihani inaonesha kuwa, mitihani hiyo iliyoanza Novemba 14 itakamilka Novemba 24 kwa watahiniwa waliopo katika shule 19 za sekondari za Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.
Pichani, mkuu wa shule ya sekondari ya Rungwempya Dickson Nussu alipokuwa na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, Novemba 18.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.