Na.Andrew Mlama.
Mwenge wa Uhuru umekamilisha ziara yake katika Halmashauri ya Kasulu baada ya kupita kwenye Miradi inayotekelezwa yenye jumla ya Thamani ya shilingi ya Tshs. 1,919,836,028/=. Katika Miradi hiyo Serikali Kuu imechangia Tshs. 937,869,500/= sawa na asilimia 49, Michango ya Wananchi ni Tshs. 96,160,592/= sawa na asilimia 5 na Wadau wa Maendeleo wamechangia Tshs. 885,805,936/= sawa na asilimia 46.
Mbio hizo zimefanyika leo tarehe 18/04/2018 ambapo umefanyika uzinduzi wa Mradi wa ujenzi wa wodi ya wazazi Zahanati ya Makere, Mradi wa maji Nyamidaho, Ujenzi wa Bwalo la chakula shule ya Sekondari Muyovozi, Skimu ya umwagiliaji Rungwempya na klabu ya kupinga na kupambana na Rushwa shule ya Sekondari Titye. Aidha umefanyika uwekaji jiwe la msingi Kituo cha Afya Nyakitonto na kufungua nyumba tano za watumishi katika Kituo cha Afya Shunga,
Mwenge wa Uhuru umepokelewa katika Kata ya Nyamidaho Wilayani hapa, ambapo katika hotuba yake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa Ndg. Charles Francis Kabeho alisema kuwa umati wa watu waliojitokeza kuupokea Mwenge wa Uhuru ni ishara tosha kuwa Kasulu kuna amani, upendo na mshikamano.
Akihutubia wakazi waliojitokeza kwa wingi katika eneo la mapokezi ya Mwenge wa Uhuru, Amempongeza Rais wa Serikali ya awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhakikisha Elimu ya Msingi mpaka Sekondari inatolewa bure “Serikali ilizuia michango katika shule zake hivyo mwalimu Mkuu au Kamati ya shule wasichangishe Michango bali ichangishwe na Kamati ya Maendeleo ya kata au vijiji kwa kufuata muongozo unaopatikana kwa Mkurugenzi’’alisema Kabeho.
Amesema Mkoa wa Kigoma haupo katika orodha ya Mikoa yenye utoro sugu. Amewataka wazazi kufuatilia mahudhurio na maendeleo ya kitaaluma ya watoto wao shuleni. Aidha amesisitiza jumkumu la wazazi kuhakikisha wananunua Sare za Shule za watoto wao kwani kutofanya hivyo ni kutotekeleza wajibu na majukumu yao.
Amewataka wananchi kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya rushwa, matumizi ya madawa ya kulevya,kupambana na kudhibiti UKIMWI pamoja na malaria.
Akisoma risala ya utii kwa niaba ya Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ndg. Mguha T.Mguha alifafanua kuwa Wananchi wa Kasulu wametekeleza ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 kwa kujenga shule za Sekondari, kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya VVU/UKIMWI, kusaidia mapambano dhidi ya malaria, kutoa elimu ya Mapambano dhidi ya rushwa na kupiga vita madawa ya kulevya.
“Kwa niaba ya Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu tunawashukuru Wakimbiza Mwenge Kitaifa, Kimkoa na Kiwilaya, Viongozi wa ngazi ya Mkoa na Wananchi wote kwa ujumla, kwa jinsi tulivyoshirikiana na kufanikisha Mbio za Mwenge wa Uhuru hapa Wilayani kwetu Kasulu’’ alihitimisha Mguha.
Mwenge wa Uhuru utaendelea na ziara yake katika Halmashauri ya mji wa Kasulu.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.