Na Mwandishi Wetu
Serikali imesema kuwa ujenzi wa maghala ya kisasa yapatayo 14 kote nchini yataliwezesha taifa kutoka hatua moja kwenda nyingine kwenye suala la usimamizi wa mazao ya chakula huku wakulima wakiwa na uhakika wa soko.
Hayo yamebainishwa juzi na Mratibu wa kudhibiti Sumu Kuvu nchini, Clepin Josephat katika Kijiji cha Nyakitonto wilayani Kasulu mkoani Kigoma kwenye makabidhiano ya miundombinu ya mradi wa uthibiti wa sumu hiyo.
Amesema ghala hilo la Nyakitonto lililogharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.1 lina uwezo kukusanya mazao ya nafaka tani 2000 kitu kitakachowasaidia wakulima kuepeukana na wadudu waharabifu baada ya mavuno.
Mkurugenzi Wa Mafunzo na Utafiti Wizara ya Kilimo, Dk Wilhelm Mafuru aliyemwakilisha Katibu Mkuu, Gerald Mweli amesema kuwa wizara imeupatia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NRFA) usimamizi wa ghala hilo kutokana na uzoefu waliokuwa nao katika masuala ya ukusanyaji wa chakula.
“ Serikali inatarajia mtatoa elimu kwa wakulima kupitia wataalamu wenu kwakuwa huwa mnanunua bidhaa ambazo ni bora, kwahiyo mtatumia wataalamu wenu kuwasaidia wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo,” alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya hiyo, Emmanuel Ladislaus aliiomba wizara kuangalia maeneo mengine yanayoweza kujengwa maghala kutokana na jiografia ya eneo hilo kuwa na uzalishaji mkubwa wa mazao ya nafaka.
“ Wilaya yetu ni moja ya wilaya zinazozalisha nafaka kwa kiasi kikubwa jaribuni kuangalia suala la kutujengea maghala kwakuwa tuna uzalishaji mkubwa kwahiyo niwaombe serikali mtuongezee idadi yake,” amesema.
Diwani wa Kata ya Nyakitonto, Daniel Mzababa amesema kuwa uwepo wa ghala hilo utasaidia kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao yao kwakuwa kijiji hicho kinaongoza kuhudumia wafanyabiashara kutoka nchi za Kenya, Burundi, Rwanda na Uganda wanaofuta bidhaa za nafaka.
Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na Mfuko wa Dunia wa Kusaidia Usalama wa Chakula (GAFSP) tayari imejenga maghala 12 Tanzania Bara na mawili Zanzibar yenye thamani ya shilingi bilioni 14.3 kwa ajili ya uhifadhi wa chakula.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.