Na Mwandishi Wetu
Halamshauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kupitia idara ya elimu sekondari imefanikiwa kushika nafasi ya kwanza kimkoa katika mtihani wa kidato cha sita kwa mwaka 2023.
Hayo yamebainishwa na Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Rebeka Harmon kwenye Kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika jana kilichojikita kujadili mapendekezo ya mpango wa bajeti ya mapato na matumizi pamoja na miradi ya maendeleo kwa mwaka 2024/2025.
Amesema tofauti na mafanikio hayo pia idara ya elimu ya msingi kwa mwaka huo walifanikiwa kushika nafasi ya pili kimkoa katika mtihani wa darasa la saba na kujenga taswira nzuri kwenye halmashauri linapozungumziwa suala la taaluma.
Aidha, Rebeka amebainisha kuwa halmashauri imefanikiwa kupima eneo la hekari 49 kwa kampuni ya TACECO kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha Saruji uwekezaji unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka 2024.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Joseph Kashushura ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho amewataka wakuu wa idara na vitengo kutambua kuwa kuna jicho la tatu linaloangalia utendaji kazi wao ambalo ni vyama vya wafanyakazi.
“Niwakumbushe watumishi tuwe na vikao kama hivi kwa ajili ya kuwekana sawa kiutendaji, hapa si kwamba tunapigana madongo bali tunajiboresha tuweze kusonga mbele ili wale wanaotuangalia kwa nje waone tunafanya kazi vizuri,” amesema.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Mageni Pondamali amewataka watumishi wa afya kuwa na lugha nzuri kwa wateja pamoja na kujiepusha na vitendo vya rushwa na ulevi uliopindukia.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) mkoani humo, Johnson Muyombya amesema kikao hicho majadiliano yake yametoa mwanga katika kutatua kero za wafanyakazi.
Tofauti na TALGWU kikao hicho pia kilikuwa na wawakilishi kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) pamoja na Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.