Na Mwandishi Wetu, Kasulu
Imeelezwa kuwa 88% ya watu hutumia teknolojia zisizoboreshwa kupikia ambazo si salama kwa afya kitu kinachopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira na kupelekea mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamebainishwa na Afisa Tarafa ya Buyonga, Paul Ramadhan leo Ijumaa Agosti 30, 2024 alipo muwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kasulu,Mhe. Kanali Isaac Mwakisu katika hafla ya uzinduzi wa Programu ya Mawasiliano ya Mabadiliko ya Tabia 'Behaviour Change Communication' inayosimamiwa na shirika la maendeleo la Uholanzi (SNV).
Na kuongeza kuwa uwepo wa programu hiyo ni mpango wa kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwa lengo la kupunguza matumizi ya nishati na teknolojia zisizo safi kwa kupikia kupitia matumizi ya majiko sanifu, kuongeza uelewa juu ya njia bora za mapishi pamoja na matumizi ya teknolojia safi na Salama.
“Kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanyika, taarifa zinaonesha kuwa matumizi ya majiko yasiyo rafiki kwa mazingira yanachangia kwa kiasi kikubwa matatizo ya kiafya pamoja na ukataji holela wa miti huku zaidi ya watu 33,000 wakifariki kila mwaka nchini Tanzania kutokana na matumizi ya nishati zisizofaa”, amesema.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Emmanuel Ladislaus amesema kuwa mradi huo umejikita zaidi katika kuhakikisha uhifadhi wa mazingira unafanikiwa.
“Ndugu zangu mazingira ndio uhai wetu hii mikakati yote inayofanywa na wadau wetu ni kuhakikisha kwamba inaisaidia serikali kufanikisha lengo la sera ya taifa ya kuboresha maisha ya wananchi kupitia matumizi ya nishati za kupikia za kisasa”, amesema.
Kwa upande wake Afisa Mazingira wa Halmashauri hiyo, Hassan Liangwana ameeleza kuwa wapo katika mkakati wa kuhakikisha kuwa 80% ya wananchi wa halmashuri husika wanatumia nishati na teknolojia safi za kupikia ifikapo mwaka 2030.
Aidha, amesema kuwa ni muhimu kutekeleza jitihada hizo kwa wananchi kuhamia katika matumizi ya nishati nyingine kwa ajili ya kupikia ikiwemo gesi asilia, gesi oevu na umeme ili kuepukana na uharibifu wa mazingira na matatizo ya kiafya yanayohusiana na moshi.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.