Na Mwandishi Wetu,Kasulu
Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu wamempongeza Mkurugenzi Mtendaji wao, CPA Francis Kafuku, kwa uamuzi wake wa kutenga muda wa kutembelea maeneo yao ya kazi na kusikiliza changamoto wanazokabiliana nazo moja kwa moja.
Pongezi hizo zimetolewa leo, Alhamisi Agosti 14, 2025, ikiwa siku ya nne ya ziara yake, ambapo CPA Kafuku amekutana na watumishi wa kata za Kalela, Kwaga na Rusesa.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Kakirungu, Anna Kaaya, amesema ziara kama hiyo ikifanyika pia kwenye ngazi ya jamii itasaidia kutoa elimu zaidi kuhusu masuala ya ufundishaji na ujifunzaji, pamoja na kupambana na changamoto kama utoro wa wanafunzi.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Msingi Kwaga, Elizabeth Ngobei, amesema hatua hiyo imeonesha mshikamano wa kweli kati ya Mkurugenzi na wafanyakazi wake, na kwamba imewapa faraja kujua wanaweza kumfikia moja kwa moja endapo wakikumbana na changamoto.
Naye Mtendaji wa Kata ya Kalela, Hassan Makwepa, ameeleza kuwa ziara hiyo imewasaidia watumishi kuwasilisha kero zao na kupata majibu papo hapo, jambo linalopunguza gharama na muda wa kufuata suluhu katika makao makuu ya wilaya.
Akihitimisha kikao hicho, CPA Kafuku amewapongeza watumishi kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii licha ya changamoto mbalimbali, ikiwemo mapunjo ya mishahara na fedha za likizo.
“Niwapongeze kwa kujituma bila kukata tamaa. Changamoto tulizoweza kuzitatua tumefanya hivyo mara moja, na zile zilizo nje ya uwezo wetu tumezichukua kwa ufuatiliaji zaidi,” amesema.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.