HALMASHAURI ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, imetoa pikipiki 10 kwa watendaji wa kata zilizonunuliwa kutokana na pesa za Mapato ya ndani, anaripoti Respice Swetu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki hizo, mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu, amewataka watendaji hao kuzitunza pikipiki hizo na kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuongeza tija na kuboresha utendaji kazi.
Mwakisu aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amewataka watendaji hao kujiepusha na matumizi yasiyo sahihi ikiwa ni pamoja na kuendesha bila kuwa na leseni.
Amesema kumekuwepo na taarifa kuwa ajali nyingi zinazotokea barabarani, husababishwa na madereva wanaoendesha vyombo vya serikali hivyo hatarajii hali hiyo kutokea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu
Joseph Kashushura, ameonesha matumaini makubwa kuwa, kununuliwa kwa pikipiki hizo, kutaboresha ukusanyaji wa mapato na kurahisisha ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo iliyopo kwenye vijiji na kata.
“Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu imekuwa ikitekeleza maelekezo ya serikali kuhusu kutumia sehemu ya pesa zitokanazo na mapato ya ndani katika maeneo mbalimbali ikiwemo kulipa posho za watendaji wa kata, sisi tumekwenda mbali zaidi kwa kuwanunulia na pikipiki”, alisema.
Kashushura alizitaja kata zilizopata pikipiki kuwa ni Kitanga, Asante Nyerere, Kwaga, Kurugongo, Kalela, Kigembe, Shunguliba, Heru Ushingo, Titye na Makere na kuahidi kuwa zilizobaki zitanunuliwa awamu ya pili.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu (aliyesimama) akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki kwa watendaji wa kata 10 za Halmashauri ya Wilaya ya kasulu, kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Halmashauri Joseph Kashushura na kulia kwake ni afisa utumishi na rasilimali watu wa halmashauri hiyo, Michael Magesa.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.