Na Mwandishi Wetu
Mafunzo ya siku nne ya uongozi wa ufundishaji na ujifunzaji kwa Waratibu wa Jumuiya za Kujifunza (JZK) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu yamehitimishwa leo, ambapo washiriki wameahidi kutumia maarifa waliyopata kuwawezesha walimu wenzao kuboresha mbinu za ufundishaji darasani na kuimarisha ukusanyaji wa takwimu za elimu.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kwaga, Andrea Chisongela, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kuelewa kwa kina namna ya kuunda dira na dhima ya shule kupitia maono ya kiongozi husika, jambo litakalosaidia kuboresha utendaji wa taasisi za elimu kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kumlama, Thimothy Mwakibala, amebainisha kuwa amejengewa uwezo wa kuendesha kwa ufanisi Mafunzo Endelevu kwa Walimu Kazini (MEWAKA) shuleni, hatua ambayo itasaidia kuinua ubora wa ufundishaji na ujifunzaji.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Heru Ushingo, Chesco Shadrack, amesema amejifunza namna ya kutumia takwimu za wanafunzi kubaini changamoto zao na kupanga mikakati sahihi ya kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mwezeshaji Jacob Chando amewahimiza washiriki kuhakikisha maamuzi wanayoyafanya katika shule zao yanatokana na tafsiri sahihi ya takwimu, ikiwemo za ufaulu, utoro na uwiano wa kijinsia.
Afisa Elimu Msingi (Taaluma) wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Joseph Maiga, ambaye alifunga rasmi mafunzo hayo, amesema programu hiyo imekuwa chachu muhimu kwa waratibu hao, kwani imewapa uelewa mpana utakaowawezesha kuboresha usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji katika shule wanazozisimamia.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.