Jengo la choo cha kisasa kilichojengwa katika shule ya Msingi Asante Nyerere.
Walimu na wanafunzi katika shule ya msingi Asante Nyerere iliyopo katika kata ya Asante Nyerere wilayani hapa, wamepongezwa kwa matumizi bora ya vyoo vya kisasa vilivyojengwa na Serikali shuleni hapo.
Pongezi hizo zimetolewa na afisa elimu ufundi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Bw. Gerard Nkona akiwa katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ambayo imefanywa na wajumbe wa Kamati ya Fedha Uongozui na Mipango ya wilaya. “Ni nadra kwa wanafunzi wenye umri mdogo kutumia vyoo vya kisasa kwa usahihi tena wakiwa katika idadi kubwa wakati matundu ni machache” alisema Nkona.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bw. Edwin Nduhire amesema ujenzi wa choo hicho umegharimiwa na Fedha kutoka Serikali kuu (P4R) ambapo Jumla ya Shilingi 6,600,000/ zimetumika kukamilisha ujenzi wa vyoo hivyo. Alisema kuwa, upo mkakati wa kujenga matundu mengine kumi kwa nguvu za wananchi ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa matundu ya vyoo kwani shule ina jumla ya wanafunzi 1771.
“Pamoja na changamoto za uhaba wa walimu, madarasa na matundu ya vyoo, shule ya msingi Asante Nyerere imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma katika matokeo ya darasa la Saba. Mwaka 2016 iliongoza kwa kuwa ya kwanza kiwilaya ambapo mwaka 2017 ilishika nafasi ya 8” alihitimisha Nduhire.
“Diwani wa kata hiyo Mh.Elias Masende amewaomba wananchi waendelee kujitolea kwani maendeleo yanaletwa na wananchi wenyewe. nitajitahidi kusimamia kwa nguvu zote kuhakikisha michango ya wananchi inatumika kama ilivyopangwa” alisisitiza Masende.
Kaimu afisa Mipango, Takwimu na ufuatiliaji Wilaya ya Kasulu Bw. Fadhili Juma amesema kuwa, ameridhishwa na ujenzi wa vyoo hivyo, hali ya usafi iliyopo na amesisitiza elimu ya matumizi bora ya vyoo iendelee kutolewa shuleni hapo ili kudumisha Afya za wanafunzi wanaotumia vyoo hivyo.
Naye Mkuu wa Idara ya usafi na mazingira wilaya Bw. Nimrod Kiporoza amesema wamekuwa wakitoa elimu ya matumizi bora ya vyoo na usafi wa mazingira kwa walimu na wanafunzi ili kudumisha mazingira safi na salama katika maeneo ya kufundishia na kujifunzia. Ameitaka Jamii kuzingatia na kudumisha utaratibu wa kuweka mazingira safi wakati wote.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.