Na Mwandishi Wetu
Walimu wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuacha kufundisha kwa mazoea na badala yake wahakikishe wanawapa watoto ujuzi na si kuharakisha kumaliza mada (Topics) ili kupandisha kiwango cha ufaulu.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatatu Juni 3, 2024 wilayani humo na Naibu Katibu Mkuu OR TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde alipokuwa anaonge na walimu hao katika ukumbi wa Chuo Cha Ualimu Kabanga.
Amesema ili kufanikisha mkakati wa serikali wa kuongeza ufaulu ni lazima wazingatie misingi minne ya ufundishaji inayojumuisha uwezo alionao mtoto, mazingira wanayopatia elimu, umri waliokuwa nao ili ujue unaenda nao vipi pamoja na utayari wa kupokea unachokitoa kwao.
“F yoyote ni ya mwalimu si mwanafunzi KPI ya kila mwalimu ni kuhakikisha kwenye somo lako hakuna F…ukiangalia ukaona walimu waliokutangulia wamefanya makosa rekebisha kwa kufanya hivyo hawataona kile unachowafundisha ni kigumu,” amesema.
Aidha, ameelekeza walimu wa shule za sekondari kuhakikisha wanafunzi wanapojiunga na kidato cha kwanza wanawajengea ujuzi wa kujua lugha ya kiingereza kwa kuandika, kuzungumza, kuelewa na kusoma alafu mchakato wa kuufundisha masomo mengine ndio uendelee.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Theresia Mtewele akizungumza katika tukio hilo amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele elimu hasa katika mkoa wa Kigoma kwa kuleta pesa nyingi zilizosaidia kuboresha miundombinu ya ufundishaji.
“Halmashauri ya Wilaya Kasulu imeletewa pesa nyingi zilizosimamiwa vizuri na walimu miradi imetekelezeka kweli kweli …na sasa tunakwenda na ajenda nyingine miundombinu ipo ni jukumu letu walimu kuhakikisha tunazingatia viwango vya ubora wa elimu ili miradi hii iweze kuleta tija,” amesema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Ndelekwa Vanica amesema kuwa halmashauri itahakikisha inatekeleza yale yote waliyoagizwa ili kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu na matokeo yake yataonekana.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.