Na Mwandishi Wetu, Kasulu
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Ndelekwa Vanica, amewataka wajumbe wa Kamati ya Lishe ngazi ya wilaya kuhakikisha kila mmoja anaandaa na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake kwa kila robo ya mwaka, ikionyesha hatua zilizochukuliwa katika kupambana na tatizo la utapiamlo.
Vanica alitoa wito huo jana, Jumatatu Agosti 11, 2025, wakati akifunga kikao cha kamati hiyo kilicholenga kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli za lishe kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Amesema utaratibu huo utarahisisha ukusanyaji wa taarifa katika sehemu moja na kutoa taswira ya pamoja kuhusu kazi zilizotekelezwa na kila mjumbe katika kipindi husika.
“Kila mjumbe aandae taarifa ya kile alichokifanya katika robo husika ili tuweze kupata taarifa ya pamoja. Sasa hivi tumemaliza robo ya nne ya mwaka wa fedha uliopita na tunaingia robo ya kwanza (Julai–Septemba). Tusiseme muda bado upo, kila mmoja apambane kutimiza hili,” amesema Vanica.
Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Lishe wa Halmashauri hiyo, Anna Njoka, amesema kuwa katika kipindi cha utekelezaji wa afua za lishe, jumla ya watoto 31 walipatiwa matibabu ya utapiamlo mkali. Amesisitiza kuwa Halmashauri itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa chakula na dawa kila robo ya mwaka ili kuimarisha huduma hizo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.