Na Mwandishi Wetu
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Theresia Mtewele, amesema wadau wa maendeleo katika sekta ya kilimo wanapaswa kushirikiana na serikali ili kusaidia wakulima kufanya kilimo chenye tija, jambo litakalosaidia kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya halmashauri na kuongeza kipato cha wananchi.
Ametoa kauli hiyo leo, Septemba 30, 2025, wakati akifunga kikao cha wadau wa kilimo wa Mkoa wa Kigoma, ambapo amebainisha kuwa usalama wa chakula katika mkoa huo uko vizuri kutokana na hamasa inayotolewa kwa wakulima, na hivyo akasisitiza wadau waendelee kushirikiana na serikali katika kuimarisha sekta hiyo.
“Niwaombe muendelee kushirikiana na serikali kwakuwa tumeelekezwa kuhamasisha ukusanyaji wa mapato, na katika mkoa wetu kilimo ndicho kinachochangia kwa kiasi kikubwa,” amesema Theresia.
Aidha, amewataka wadau hao kutumia kipindi hiki cha maandalizi ya bajeti kuweka maazimio muhimu ili kuepuka changamoto wakati wa utekelezaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, amesema kuna umuhimu wa kuanzisha jukwaa la kudumu la wadau wa kilimo kwa ajili ya kuonyesha bidhaa na shughuli zao badala ya kutegemea maonesho ya Nanenane pekee.
Awali, Mwenyekiti wa Maafisa Kilimo wa Mkoa wa Kigoma, Keneth Tefurukwa, alisema kikao hicho kimebaini changamoto mbalimbali na namna ya kuzitatua, na hivyo wamejipanga kuyafanyia kazi maazimio yote yaliyofikiwa.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.