Na Mwandishi Wetu
Wadau wa kilimo mkoani Kigoma leo, Septemba 29, 2025, wamekutana wilayani Kasulu kujadili njia za kuimarisha ushirikiano ili kutumia rasilimali zilizopo kwa maendeleo ya kilimo chenye tija na uhakika wa soko.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Katibu Tawala Msaidizi wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji mkoani humo, James Peter, amesema jukwaa hilo linatoa fursa kwa wadau kuwasilisha tathmini ya utekelezaji wa shughuli zilizopita na kueleza mikakati ya mwaka huu.
“Kila mdau ana mchango wake katika sekta ya kilimo. Tunapokutana tunashirikishana, tunashauri na kuongeza mashirikiano ili kutumia rasilimali zilizopo, ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa masoko ya uhakika,” amesema.
Kwa upande wake, Kilio Mnyoreka kutoka Mradi wa Youth Entrepreneurship for the Future of Food and Agriculture (YEFFA), amesema wamewezesha vijana kutoegemea masoko ya ndani pekee kwa kuwapatia taarifa sahihi za masoko mengine, jambo linalowawezesha kuuza bidhaa zao maeneo mbalimbali.
Naye Afisa Kilimo wa Mamlaka ya Uthibiti Mazao ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Mary Mlay, amebainisha kuwa mikakati yao mkoani Kigoma inalenga kutafuta wawekezaji katika zao la muhogo ili kuongeza thamani na kupanua soko, ikiwemo kuuza bidhaa nje ya nchi.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.