Na Mwandishi Wetu
Ili kukabiliana na ugonjwa wa Kipindupindu waratibu wa shughuli mbalimbali za kiserikali wilayani Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuhakisha maeneo wanayoyasimamia yanakuwa katika hali ya usafi ikiwemo takataka kuondolewa kwa wakati sehemu zinapohifadhiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu ameyabainisha hayo hivi karibuni kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC).
Kikao kilichokuwa na lengo la kuibua vyanzo vipya vya mapato ili vipate kujumuishwa kwenye bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
“Kasulu ama Mkoa wa Kigoma tumepakana na mikoa yenye viashiria vya ugonjwa wa Kipindupindu na ugonjwa huu wote tunatambua unasababishwa na uchafu, sasa Kasulu inakuwa uzalishaji wa taka umekuwa mkubwa tusipokuwa makini kuzidhibiti tutaingia kwenye matatizo ya Kipindupindu” amebainisha.
Aidha, Mwakisu aliwataka watendaji wa kata kuhakikisha watoto wanaandikishwa kujiunga na elimu ya msingi pamoja na ile ya sekondari.
“Nataka watoto waende shule kwa mujibu wa TAMISEMI watoto wa ‘form one’ wanatakiwa kuripoti mwisho mwezi wa tatu tarehe 30 lakini mimi sitaki kufika huko,” amesema.
Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Kasulu, Eliya Kagoma aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuja na kauli mbiu ya kupambana na vitendo vya ramli chonganishi maarufu kama Kamchape.
“Muheshimiwa Mkuu wa Wilaya napendekeza kama ikikupendeza tuwe na falsafa ambayo watu wa afya walikuwa wanasema Malaria haikubaliki tushirikiane kuitokomeza…nilikuwa nimewaza wazo tutembee na kauli mbiu kwamba Kamchape haikubaliki tushirikiane kuitokomeza,” amebainisha.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya hiyo, Mbelwa Chidebwe alishauri kuwepo na usimamizi mzuri wa shughuli za ukusanyaji mapato ili malengo yaliyowekwa na halmashauri yaweze kutimia kwa mwaka huo wa fedha.
Kikao hicho kiliudhuriwa na wajumbe kutoka kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, viongozi wa vyama vya siasa, maafisa wa serikali, wakuu wa idara wa halmashauri hiyo, taasisi za kifedha, mashirika ya kimataifa na wadau wa zao la Pamba na Tumbaku.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.