Na Mwandishi wetu
Viongozi wa ngazi ya vijiji na vitongoji wilayani Kasulu mkoani Kigoma wameagizwa kujiepusha kuchochea migogoro ya wakulima na wafugaji.
Ambapo wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu ikiwemo kutoruhusu kisheria uingizwaji wa idadi kubwa ya mifugo katika maeneo yao.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,Thobias Andengenye alipozungumza na wakazi wa Kata ya Nyamidaho wilayani humo,alipofanya ziara ya kikazi iliyolenga kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero zao.
"Nyinyi viongozi kuanzia ngazi ya vijiji acheni kutoa vibali vya kuruhusu mifugo kuingia katika maeneo yenu ya kiutawala huku mkijua wazi kuwa hakuna sehemu za malisho kutokana na maeneo yaliyopo kutumika kwa shughuli za kilimo," amesema.
Ameelekeza wafugaji kupeleka mifugo yao katika maeneo yaliyotengwa na Serikali kwa ajili ya malisho kufuatia kuwepo kwa malamiko ya wakulima kuwa wanachungia katika mashamba yao.
"Wapo wafugaji kutoka nje ya mkoa wamekuwa wakionesha uhitaji wa matumizi ya maeneo tengefu kwa ajili ya malisho ya mifugo lakini tumedhamiria kutoruhusu ili nyinyi mliopo mkatumie maeneo hayo na kuondoa migogoro," amesisitiza.
Katika hatua nyingine Andengenye amewahasa wazazi wa kata hiyo kukaa karibu na watoto wao kuanzia kipindi cha ujauzito hadi wanapokuwa ili kuwajengea siha na tabia njema siku za mbeleni.
"Hakikisheni mnapendana huku mkiwapenda watoto wenu na mojawapo ya kigezo hicho ni kuona wanapata haki yao ya utambulisho wa kuzaliwa," ameshauri.
Pamoja na hayo pia ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanafuatilia maendeleo ya watoto wao mashuleni ili wapate ufaulu mzuri katika ngazi mbalimbali za kitaaluma wanazopitia.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.