Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu (aliyesimama) akizungumza katika kikao cha viongozi wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Kigoma kilichofanyika Wilayani Kasulu, walioketi ni Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Kigoma Feruzi Mbaya (kushoto);na Katibu wa CCM Mkoa wa Kigoma Mobutu Malima.
MKUU wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu, amewatahadharisha wakazi wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kukwamisha zoezi la anuani za makazi.
Kauli hiyo ameitoa katika kikao kilichowahusisha viongozi wa Chama cha Mapinduzi wa mkoa wa Kigoma walipokuwa wakihitimisha ziara ya siku mbili Wilayani Kasulu.
Mwakisu ametoa kauli hiyo kufuatia baadhi ya hoja zilizowasilishwa katika kikao hicho kuhusu migogoro ya mipaka iliyopo katika vijiji na mitaa ya wilaya ya Kasulu.
Amesema kuwa, mipaka hiyo kamwe isihusishwe na anuani za makazi na atakaposikia kuna mtu yeyote katika Wilaya hiyo amesababisha kukwama kwa zoezi la anuani za makazi, atamchukulia hatua kali ikiwa ni pamoja na kumweka ndani.
“Rais wetu amekwisha toa pesa nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi la anuani za makazi, siko tayari kusikia kuwa kuna mtu anakwamisha zoezi hilo”, alisema.
Akizungumzia suala la wakimbizi wanaoingia nchini bila utaratibu, Kanali Mwakisu amewataka wakazi wa Wilaya ya Kasulu kushirikiana na serikali katika kukabiliana na tatizo hilo badala ya kuitegemea idara ya uhamiaji na vyombo vya usalama pekee kwa kuwa jukumu la ulinzi na usalama wa nchi ni la kila raia.
Ameongeza pia kuwa, tatizo la wahamiaji kutoka nchi jirani ni moja ya matatizo makubwa yaliyopo katika Wilaya ya Kasulu hivyo vyombo vya ulinzi pekee havitaweza kutokana na ukubwa wa tatizo hilo.
Awali katika kikao hicho, Katibu wa Chama cha Mapinduzi wa mkoa wa Kigoma Mobutu Malima, amewaasa wataalamu na viongozi wa siasa Wilayani Kasulu kushirikiana kwa pamoja katika kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Amesema kuwa, kazi ya viongozi wa Chama ni kuhakikisha kuwa ilani ya Chama inatekelezwa na kazi ya wataalamu ni kutekeleza ilani ya Chama.
Aidha, Malima ambaye ziara hiyo ni ziara yake ya kwanza Wilayani Kasulu tangu ateuliwe kushika wadhifa huo mwishoni mwa mwaka jana, ametoa pongezi kwa viongozi wa Wilaya hiyo kwa kazi wanazofanya.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya mji wa Kasulu, kimewakutanisha wataalamu, wanasiasa na madiwani wa Halmashauri na mji wa Kasulu.
Picha ya pamoja ya viongozi wa Chama cha mapinduzi na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.