Na Mwandishi Wetu, Kasulu
Matumizi ya Mfumo wa kielektroniki wa Kuratibu Vikao vya Bodi na Menejimenti (e-Board) yamelenga kuongeza ufanisi wa uandaaji na uendeshaji wa vikao kitu kitakachosaidia kupunguza gharama za maandalizi yake.
Afisa TEHAMA wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Jamal Sempoli amebainisha hayo leo Jumatatu Oktoba 28,2024 alipokuwa mwezeshaji kwenye mafunzo ya utumiaji wa mfumo huo kwa wakuu wa divisheni na vitengo wa halmshauri hiyo.
“Mfumo tukiufahamu vyema utasaidia halmashauri kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zinatumika kuandaa makabrasha kwakuwa taarifa zote hizo zitakuwa katika mfumo na madiwani na wataalam kuwa na uwezo kuzipakua huko,” amesema.
Kwa upande wake mwezeshaji mwingine wa mafunzo hayo, Fiona Emmanuel amesema kuwa mfumo huo utasaidia kuokoa muda na gharama za kusambaza makabrasha kwakuwa hivi sasa inawalazimu kuyafikisha katika kata zote 21 zilizopo katika halmashauri.
Afisa Biashara wa Halmshauri ya Wilaya ya Kasulu,Renaltus Kavishe amesema mfumo huo ukieleweka vizuri utasaidia kurahisisha mawasiliano baina ya watumishi kwa watumishi au watumishi na madiwani kwakuwa mambo yote muhimu yanayowahusu yapo ndani.
Naye Mkuu wa Idara ya Afya,Lishe na Ustawi wa Jamii wa halmshauri hiyo, Dkt. Chacha Tubeti amebainisha kuwa e-Board itasaidia idara kuwa na uwezo wa kupata taarifa mapema popote mtumiaji atakapokuwa kitu kitakachoboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.