Na Mwandishi Wetu
Timu ya madaktari bingwa wa magonjwa saba tofauti kutoka hospitali mbalimbali hapa nchini, inayojulikana kama “Timu ya Mama Samia”, imeweka kambi ya matibabu ya kibingwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, iliyopo Nyamnyusi. Lengo kuu la kambi hiyo ni kusogeza huduma za afya za kibingwa karibu na wananchi, hasa waliopo maeneo ya vijijini.
Akizungumza hospitalini hapo leo, Dkt. Agustino Maufi mmoja wa madaktari bingwa waliopo katika kambi hiyo amesema kuwa timu hiyo imejumuisha wataalamu wabobevu wa magonjwa ya ndani, watoto, kinywa na meno, upasuaji, usingizi na ganzi, pamoja na muuguzi mahiri wa afya ya uzazi.
“Tunaendelea kuwakaribisha wakazi wa Wilaya ya Kasulu kuja kupata huduma hizi muhimu. Mbali na matibabu, tunashirikiana na watumishi wa afya wa hapa ili kuwajengea uwezo na kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya,” amesema Dkt. Maufe.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Mahamudu Mitenda, amesema ujio wa madaktari hao umeleta nafuu kubwa kwa wananchi, kwani sasa wanapata huduma za kibingwa bila kulazimika kusafiri kwenda mbali, hivyo kupunguza gharama kubwa za usafiri na malazi.
Mwalimu Frederick Kamayugi, mmoja wa wananchi waliopata huduma, amesema kuwa huduma hiyo kuwafuata wananchi imekuwa msaada mkubwa kwao. “Awali tulilazimika kwenda Bugando au Muhimbili kutafuta huduma hizi, lakini sasa zinapatikana hapa hapa Kasulu. Tunashukuru sana,” amesema.
Naye Bernadeta Asheri amesema alimpeleka mwanaye katika kambi hiyo baada ya kusumbuliwa na tatizo la kiafya kwa muda mrefu. “Madaktari wametuhakikishia kuwa wanaweza kumtibu, na tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea huduma hii ambayo imetupunguzia gharama kubwa,” amesema.
Katika maoni mengine, Mawazo Itibari amesema kuwa baada ya kupata ushauri kutoka kwa madaktari bingwa, sasa ana matumaini ya kupona bila kulazimika kwenda Mwanza au Dar es Salaam. “Ni afueni kubwa kwetu sisi wananchi wa maeneo haya,” ameongeza.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.